Ads Here

Saturday, September 21, 2019

*NYUMA YAKO --- 02* *Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Na kwasababu haujayapa kipaumbele kama yale ya mbele, mambo haya ya nyuma huwa ya ghafla na hatarishi zaidi, yakikuacha ukiwa umelala chini hujiwezi, damu zakububujika.

Tazama nyuma yako. Huenda kuna mchezo unaendelea ambao hauuoni.

ENDELEA

SURA YA PILI …

Ni kwa muda mfupi kwa kadiri tulivyoweza tukawa tumefika Marekani, New York. Safari hiyo ni ya umbali wa masaa kumi na tano na dakika thelathini na tatu. Lakini kwasababu ya mambo ya masaa, kijografia Hong Kong ipo mbele kimajira kuliko Marekani hivyo tukafika siku hiyo hiyo tuliyotokea Hongkong, Jumatano, huku Marekani yakiwa ni majira ya mchana.

Ni ajabu enh? Basi ili tusipotazane hapa, maana kuna mikanganyiko zaidi huko mbele, acha tueleweshane kwa ufupi. Dunia huzunguka toka Magharibi kuelekea Mashariki, kwahiyo basi upande wa Mashariki huwai kuliona Jua kuliko ule wa Magharibi. Tupo pamoja?

Kwahivyo basi, ukiwa Hong Kong unatangulia kuliona na kulichoka jua kabla hata Marekani hawajaliona. Na wakuta Hong Kong ikiwa ni Jumatano, bado Marekani ni Jumanne au Jumatatu usiku baadhi ya maeneo machache ya Magharibi ya mbali. Kwahiyo kusafiri kutoka Hongkong kwenda Marekani, ni safari unayopoteza muda, yaani badala ya muda kuongezeka, unakuwa unapungua maana umetoka Mashariki kurudi Magharibi ambapo kupo nyuma kimasaa.

Natumai umenielewa.

Lakini hapa New York si ambapo tulikuwa tunaelekea. Makao makuu ya CIA yapo Virginia, umbali wa maili mia nne na nane toka jiji la New York. Kwa mwendo wa basi ingetugharimu masaa saba kasoro, hatukuwa na muda huo wa kupoteza kwahiyo ikatulazimu kuchukua ndege ili angalau tutumie lisaa limoja na robo hivi kufika Virginia.

Tukafanya hivyo, pasipo kupumzika, tukafika Virginia majira ya saa tisa alasiri. Nikamwacha Jack Pyong na mpenzi wake mie nikienda mpaka makao makuu kukutana na Inspector General, bwana Ethan Benjamin, mwanaume wa makadirio ya miaka hamsini kasoro haba.

“Karibu, Marshall,” akanikaribisha akinionyeshea kiti. Nikaketi na kumtazama. Alikuwa tayari ananitazama kwa umakini kana kwamba mwalimu wa usafi akitafuta kasoro kwenye sare ya mwanafunzi.

Bwana Ethan ni mtu mmoja mpole sana. Ni mara chache sana utamsikia akipaza sauti yake. Hupenda kutumia macho na maneno machache tu haswa akikukumbusha juu ya uwepo wako kwenye taasisi nyeti kama hiyo, CIA.

Mara kadhaa amekuwa akisema kabla ya kuwaruhusu maajenti wakafanye kazi zao, CIA ni moyo wa Marekani, hivyo msifanye taifa kuwa mfu.

Ni ngumu sana kumjua kama yupo kwenye msongo wa mawazo ama furaha. Uso wake ni mfichavi mzuri sana wa hisia. Najaribu sana kuwa kama yeye, lakini naishia kushindwa. Haswa nikiwa na mpumbavu Jack Pyong.

Akasafisha koo lake na kuniambia, “Marshall, nina kazi kubwa sana ya kukupatia. Najua hautaniangusha.” Akili yangu ikaanza kuwaza itakuwa kazi gani hiyo ya kunitoa kwenye likizo yangu na kuitwa moja kwa moja na Inspector General? Ndivyo tulivyofundishwa. Yakupasa kuwaza ya mbele, hata kubashiri kwa mantiki pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa.

Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa pia kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkuu wangu wa kazi.

“Hapa tuongeapo, Raisi amepotea,” akasema kisha akanyamaza akin’tazama kwa kunisoma. “Alikuwa njiani akielekea Berlin, Ujerumani, kwenye mkutano wa mataifa makubwa kiuchumi, lakini mpaka sasa tuongeapo hajulikani alipo, na inasemekana ndege yake imeanguka huko mbali ya bahari ya Pasifiki.”

Kauli hiyo ikatosha kunitoa macho kwa mshangao. Nikajitengenezea vema kitini na kumtazama Mkuu akinena.

“Taarifa haijatangazwa rasmi, lakini haiwezi kukaa kabatini kwa muda. Hili laweza kuwa shambulizi la kigaidi, nina mashaka nalo. Na mpaka kukuita hapa maana yake ni kwamba nina mashaka nalo.”

Akanyamaza na kunitazama kwa sekunde mbili, alafu akaniita, “Marshall.”

“Ndio, Mkuu.”

Akasema, “Nishatoa maelezo haya kwa mkuu wako wa kitengo. Unachotakiwa kukifanya ni kwenda kumtafuta Raisi popote alipo. Kama amekufa, tuletee mwili wake hapa niamini. Na pia … vichwa vya hao waliohusika!” akiwa anasema hayo maneno ya mwishoni alikuwa anaminyia kidole chake juu ya meza, macho akiyakaza.

Kwa kuongezea zaidi akaniambia nitashirikiana na inspekta wa FBI (Federal Bureau of Investigation) Miss Danielle James kuhusiana na chochote kile cha upelelezi ntakachokihitaji ndani ya nchi. Hii ni kwasababu CIA huwa wanahusika zaidi na mambo ya nje, nchi za kigeni, wakati FBI wao wakihusika na intelijensia ya ndani ya nchi, kukusanya taarifa, ushahidi, na kushurutisha sheria.

Hivyo kuna nyakati huwa tunategemeana kutekeleza majukumu yetu.

“Utamkuta hapo nje,” akasema mkuu na kumalizia tena, “Usiniangushe, Marshall. CIA ni --”

“Moyo wa Marekani,” nikamsaidia kumalizia kisha nikatikisa kichwa na kutoka nje ya ofisi. Nikakutana na Danielle, mwanamke mkakamavu mwenye nywele nyekundu akiwa amevalia suti rangi ya kahawia. Akanisalimu nami pia nikamsalimu kisha nikaenda kukaa naye kwa ofisi yangu kwa muda mchache mno, nikionelea ni kheri kwanza niende kwenye eneo la tukio kumtafuta Raisi, alafu nitakuja kurejea kuongea naye zaidi.

“Kwahiyo unaonaje?” akaniuliza. Kwakweli sikuwa najua nini ametoka kuongelea, kwani mawazo yangu yalikuwa mbali kidogo. Nilikuwa najaribu kuwaza ni wakina nani watakuwa na ‘guts’ za kufanya tukio kubwa kama hilo? Na amewezaje kufanya vivyo ingali ulinzi wa Raisi huwa ni wa hali ya juu?

“Daniella, tutaonana. Sawa?” nikamuaga nikinyanyuka kuuendea mlango, nikaufungua na kumtazama. Mwanamke huyo akatikisa kichwa kabla hajanyanyuka na kujiendea zake. Mimi nikarejea pale kitini na kuwaza kwa muda kidogo juu ya namna ya kuenenda. Punde nikatungua koti langu jeusi lililopo ndani ya ofisi, nikaliweka begani na kutoka.


**

Ni hivi, katika oparesheni kama hii, siwezi kwenda mwenyewe. Nahitaji msaada toka kwa watu wengine ambao tutaunda timu ya kufanya kazi. Ndani ya CIA kuna kitengo cha shughuli maalum, kwa jina ‘The Special Activities Centre’, kifupi SAC. Kitengo hichi kimegawanyika kwenye makundi mawili; PAG na SOG.

Oparesheni za kisiasa na kiuchumi huendeshwa na ‘The Political Action Group’, kifupi PAG. Hawa wanahusika na ushawishi wa kisiasa na wa kichumi wa Marekani dunia nzima. Na oparesheni zenye hatari ya juu kijeshi hufanywa na ‘The Special Operation Group’ kifupi SOG.

Wahusika wa SOG huwa hawabebelei nguo au kitu chochote cha kuwaonyesha kuwa wao wametokea Marekani. Na hii ni kwasababu muda wowote ule ambapo mambo yakienda kombo, basi Marekani wanaweza kukana kuhusika nao.

Ndani yake kunakuwa na watu wenye ujuzi wa hali ya juu, ambao wengi wao hutolewa kwenye kitengo cha special force au tuite komando toka jeshini. Na kwakufanya mambo kuwa mepesi na ‘manageable’ huwa wachache tu kwa kila oparesheni.

Hivyo basi kwakuwa kila kitu kilishakuwa bayana, nilipoonana na mhusika wa kitengo cha SAC (The Special Activities Centre), akanikabidhi vijana wanne kwa ajili ya kazi akiwa amefuata maelekezo ya Inspector General. Kwahiyo kutokana na kazi tuliyokuwa tunaelekea kufanya, sisi tukawa ni SOG (The Special Operation Group).

**

Ulikuwa ni usiku sasa wa saa mbili tukiwa angani ndani ya ndege ya mapambano. Tukiwa tumekaa kwa kutazamana, tukamsika rubani akitangaza kusema tunaingia eneo la tukio hivyo basi tuanze kujiandaa kwa ajili ya kuchumpa.

Tukaweka kila kitu sawa; begi la parachuti na miwani ya kutusaidia kuona usiku. Tulikuwa tumevalia nguo nyeusi za kombati zisizo na bendera, pia tumebebelea vifaa kadhaa vya kutusaidia kimapambano na kuzamia. Punde rubani aliposema tumefika, mkia wa ndege ukafunguka nasi tukarukia nje pasipo kujiuliza.

Tukachukua kama dakika sita tukiwa hewani tukibebwa na maparachuti tunasukumwa na upepo. Tulipotua, ilikuwa ni kisiwani, tukiwa tunafuata ramani, tukatembea upesi mpaka kufika eneo la ufukweni. Palikuwa kimya haswa. Nikatazama tena kwenye ramani yangu kuhakikisha. Ni kweli nilikuwa mahali ninapostahili.

Hapakuwa na alama ya kitu chochote hapo. Maji yalikuwa yanasukumwa na upepo kutengeneza mawimbi, na miti inatikisika kutengeneza muziki.

Hapa ndiyo nikajua ya kuwa sisi ni watu wa kwanza kufika hapo. Ina maana tangu Raisi aangukie maeneo hayo, hakuna mtu aliyewahi kukanyaga hapo.

**

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...