Ads Here

Friday, September 27, 2019

*NYUMA YAKO -- 05* *Simulizi za series

Nikamuuliza, "lakini mbona wewe ni wa tofauti na wenzako? Umejuaje lugha yetu?"
Akaniuliza, "hayo ndiyo maneno yako ya mwisho ukielekea kufa?" Kisha akatikisa kichwa. "Nilidhani wewe ni mwerevu."
ENDELEA
Na asiendelee kuongea nami, akashika njia aende zake. Nikamwita asijali. Akaendelea kuondoka akipiga mluzi. Lakini nilipomwambia maneno haya, akasimama.
"Nina kitu kwa ajili yako!"
Akanitazama na kisha akakunja sura kama atiaye shaka alafu akanijongea na kuniambia, "sina muda wa kupoteza nawe ewe bwana wa manjano. Ni nini hiko wataka kuniambia?"
"Kama unataka nikuambie niweke huru toka kwenye nyara hizi!" Nikamsihi. Akatabasamu na kisha kucheka kidogo kana kwamba mtu mwenye utumbo mtupu. "Unadhani mimi ni mjinga kama wewe?" Akaniuliza.
"Ujinga wangu uko wap?"
Akatahamaki, "hujioni ulivyo mjinga? Uliwaua watu wa kijiji hiki alafu ukaja tena ukiwa hujiwezi. Unadhani wewe ni mwerevu?"
"Sikuwahi kuj--"
"Ishia hapo! Siko kuskiza ngonjera zako. Kama huna cha kuniambia, acha niende kwa amani nawe ubaki hapa kutafunwa na mti!"
"Ninacho ... ninacho cha kukuambia. Na najua utafurahi ukikisikia."
Akabaki akin'tazama kwa macho ya mchoko. Hakutaka tena kusema kitu bali asikie hicho ambacho nataka kumwambia.
"Umeona ewe bwana mdogo, nina namna ya kukufanya uishi chini ya maji!"
Nikamwaona akikunja ndita za umakini kwa mbali. Hapa nikajua mada yangu imemgusa.
"Kama afanyavyo samaki, nawe utaishi, kuona na kuzamia. Je, hiko si kitu cha maana kukwambia?"
Nilitazamia jambo hilo litakuwa geni kwake. Niliomba iwe hivyo, kwani kama ingelikuwa tofauti, basi ningeambulia kuachwa nijifie. Hapana. Nilikuja hapa kumsaka Raisi na si kifo.
Akanicheka. "Unamaanisha mtungi wa hewa na mawani ya kuziba macho?" Akaniuliza akibinua mdomo. Akacheka tena mpaka akidaka magoti yake na kushikilia tumbo lake.
"Skiza ewe mtu wa manjano. Mimi si mjinga kama unavyofikiri kichwani mwako. Unadhani sijui unavyovizungumza?"
Akanipa maswali juu yake, mbona ni mwerevu kiasi hiki? Kumbe mtu huyu si tu kwamba anajua lugha yetu, bali pia na teknolojia! Hapa ilinibidi nifanye kazi ya ziada.
"Sawa, basi nitakupa cha kukufanya uone nyakati za usiku!" Nikasema kwa kujivuna. "Utatembea kama mchana usijikwae kisiki au kudumbukia shimoni!"
Hapa akanyamaza kwa muda, macho yakiwaza, alafu akaniuliza, "sasa umeona unidanganye?"
Nikajua hili kwake ni geni.
"Nidanganye ya nini na wakati naomba kubakiziwa uhai tena nikiwa nimezingirwa na maji pande zote?"
Akabinua mdomo na asiseme chochote, akaenda zake. Nikamwita asigeuke nyuma abadani mpaka anatokomea. Nikalaani sana. Nikajiuliza ni nini nitafanya na wakati mikono na miguu yangu imefungwa kwa kamba kiasi kile?
Tukio hilo likanikumbusha mbali sana. Mbali ya mwaka juzi ambapo niliagizwa kwenda kuwakomboa baadhi ya mateka wa kimarekani waliokuwa wanashikiliwa na wanamgambo wa Boko Haram huko nchini Nigeria.
Nakumbuka, nikiwa nimeambatana na wanaume wanne , wamarekani weusi, wa kikosi maalum (special forces), tukiwa mgahawani, tulizingirwa na kuwekwa chini ya ulinzi na watu sita ambao walikuwa wameficha nyuso zao na kubebelea bunduki aina ya ak 47.
Watu hawa kwa namna tulivyowatazama walikuwa ni wanamgambo wa Boko Haram, haswa kutokana na mitandio waliyokuwa wamejivika nayo usoni mbali na kombati walizovaa.
Walituamrisha tunyooshe mikono juu na kututaka tuendee gari walizokuja nazo. Tukafanya hivyo pasipo ubishi. Wakatusweka na kutimka tukielekea mahali tusipopajua kwa maana walitia vichwa vyetu ndani ya mifuko meusi.
Wakiwa wanatupeleka huko, wakawa wanateta kwa lugha ya kiarabu ambayo tulikuwa tunaisikia, wakifurahia kukamatwa kwetu na namna ambavyo wao watanufaika kwa kuongeza mateka wa kimarekani kwenye ghala.
Lakini walijuaje kama sisi ni wamarekani? Ilikuwa ni rahisi sana, na 'in fact' ni sisi ndiyo tulifanya wakatujua hivyo. Hapo mgahawani tulikuja na gari, Nissan double cabin nyeupe, yenye chapa ya USAID ubavuni. USAID ni shirika la Marekani.
Tukiwa mgahawani, tukawa tukizungumza kiingereza chetu, kiingereza cha lafudhi ya Marekani. Na zaidi mgahawa huo ulikuwa ukipatikana katika moja ya kanda ambazo ni mhanga wa mashambulizi ya mara kwa mara ya Boko Haram, kaskazini mashariki wa Nigeria, hivyo kutokea kwa wale wajamaa kilikuwa ni kitu cha kutegemewa. Kitu ambacho unaweza kukibashiri!
Wakiwa wanazungumza hayo yao, tena sisi tukiwa tunawaelewa, nasi tukawa tunazungumza kwa ishara, 'sign language' pasipo wao kuhisi wala kuelewa.
'Sign language' ama 'paralinguistic language' ni lugha isiyo na maandishi ama sauti. Ni utaalamu wa kufikisha ujumbe kwa namna ya kupeana ishara 'signals' na mwenzako akakuelewa na kujibu.
Hiki ni miongoni mwa vitu tujifunzavyo tuwapo mafunzoni kwaajili ya kujiandaa na mazingira mbalimbali ukiwa mhitaji wa kuwasiliana.
Kwa kutumia miguu yetu, tukaminyana, na pia kwa kutumia mikono yetu ambayo ilikuwa imefungwa, tukagusana kwa vidole tukifikishiana ujumbe.
Baada ya hapo, tukangoja. Mwendo wa kama nusu saa tukiwa kimya, ila sio tukiwa malofa. Mmoja wetu tulimpatia kazi ya kuhesabu majira na zoezi la kutushtua pale atakapokuwa ameona mahesabu tuliyoyapanga yametimia.
Kwa muda wa kawaida, kama tulivyokuwa tukiwaza kuwa watu hawa watakuwa wanatupeleka msitu wa Sambisa ambao ni moja ya ngome ya Boko Haram, ilikuwa yachukua kama lisaa limoja na dakika kumi na mbili endapo gari ikienda kwa mwendo wa kilomita themanini kwa lisaa.
Na kama halitoenda kwa mwendo huo, basi tena linakuwa jukumu na mpanga mahesabu kupiga mahesabu hayo kutokana na mwendo ulivyo. Kwa nilivyokuwa nahisi, gari lilikuwa linaenda kilomita mia na ishirini kwa lisaa. Sikuwa mbali na ukweli. Kidogo mahesabu yangu yalikaribiana na mkokotoaji yakiachana kwa kama sekunde kumi na sita tu!
Nikabinywa pajani. Hiyo ilikuwa ni ishara kuwa muda uliokuwa umetengwa sasa umekaribia, zimebaki sekunde nne tu. Nikabinywa na vidole vinne, vitatu, viwili, mwishowe kimoja! Kidogo gari likazama kwa korongo barabarani, hapo hapo, ndani ya dakika chache, tukanyanyuka na kutupa miili yetu mahali tulipokuwa tukisikia sauti za watu na kuhisi uwepo wao!
Ilikuwa ni kitu cha upesi na kushtukiza!
Kule kwenye bodi mulikuwa na wanamgambo sita, watatu wakikalia kushoto na watatu kulia, na basi kwasababu sisi tulikuwa watano kwa idadi, ilikuwa rahisi kuleta shambulizi lenye tija kwa kufuata mipango tuliyopanga kuwa wawili wataenda huku na watano wataenda upande mwingineo.
Ilikuwa pia rahisi kwasababu wanamgambo wale hawakuwa kwenye balansi muda mfupi baada ya gari kupitia mtikisiko. Hivyo, baada ya kufanya hivyo, nikawahisha kichwa changu kwenye mikono ya mwenzangu, akanivua mfuko kichwani.
Kutazama, nikawaona wanamgambo wawili wakiwa wanajiweka tenge kushambulia kwa risasi. Wawili walidondoka chini barabarani, wawili wengine wakiwa wameshikilia bomba la gari kutafuta balansi!
Haraka nikajitupa samasoti kwa chini kuwafuata. Nikamtengua mmoja miguu, na yule mwingine alipotaka kunishambulia, nikajikinga na mwili wa mwenzake, alafu nikampokonya bunduki yule niliyemtumia kama ngao na kisha mwili wake nikamtupia mwenziwe, wote wakadondoka chini!
Nikasikia ti-ti-ti-ti! Haraka nikajilaza chini. Kutazama nikaona mwenzetu mmoja akiwa amedondoka kwa kushindiliwa risasi! Tulikuwa tukishambuliwa na dereva.
Nikatulia na kufyatya risasi moja, ikamdungua kichwa na kummaliza papo hapo, gari likaanza kwenda mrama, lakini kabla halijaleta madhara, mmoja wetu akaliwahi na kuliweka kimyani, kisha tukaendeleza na safari kwenda huko msituni.
Basi kwakuwa wale wenzangu walikuwa na ngozi nyeusi wakajivika nguo za wale wanamgambo na kisha kuigiza kuwa wameniteka kwa lengo la kuzama ndani ya ngome.
Kwa kufupisha habari hiyo, ambayo pengine nitakuja kuisimulia vema siku nyingine, kilichonifanya niikumbuke ni namna tulivyokuta mateka wakiwa wamefungwa kamba mitini, wamarekani na wengine toka nchi za Ulaya. Na kwasababu za kioparesheni, nami nikatiwa kambani kama wale mateka wengine, lakini kamba yangu ilikuwa legevu kwa maana kwamba punde mambo yatakapoharibiwa nitoke hapo.
Ilikuwa ni tofauti na oparesheni ya Raisi kule kisiwani kwani kamba ya kisiwani ilikuwa imekazwa haswa na hakukuwa na namna ya mimi kuchoropoka isipokuwa kwa msaada. Na tofauti kabisa na Nigeria, siku hiyo wenzangu wote walikuwa hawajiwezi. Hawakupewa tiba kama ilivyokuwa kwangu, hivyo siku hiyo mimi ndo' nilikuwa na jukumu la kuwaokoa.
Muda ukaenda na giza la usiku likafika. Punde kidogo, baada ya giza hilo kuingia, nikaanza kutambua kwanini tulifungiwa kwenye miti ile mipana. Nilianza kuhisi mgongo wangu unafinywa kuzamia ndani, na kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikawa nahisi maumivu makali ya mgongo.
Nikajitahidi kujichoropoa, wapi! Zaidi nikajiongezea maumivu zaidi. Niliporusha macho kuwatazama wenzangu, nikawaona wakiwa wametulia tuli. Hawakuwa na fahamu!
Nikahisi usiku huu ndiyo mwisho wetu.

**

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...