Ads Here

Thursday, October 3, 2019

RIWAYA: NI ZAMU YAKO KUFA SEHEMU YA SITA – PART 1

Kazi ya kwanza aliyokuwa amepewa Max ni kuhakikisha anawamaliza wapelelezi wote mashuhuri katika ukanda huu wa maziwa makuu. Kazi hii peke yake ingemwingizia pesa nyingi toka kwa tajiri wake. Pili ingekuwa kuwafyeka viongozi wote ambao wangeonekana kuwa kikwazo katika kufanikiwa kwa mipango ya wazungu hao.
Ni katika kutekeleza kazi ya kwanza, ya kuwamaliza wapelelezi wote mashuhuri katika ukanda huu, ndipo mpango wa propaganda za silaha hatari ulipobuniwa. Hii ilikuwa na lengo la kuhakikisha kuwa wapelelezi wote mashuhuri katika Afrika mashariki watumwe kwenda Arusha ili kwenda kutafuta ukweli juu ya tetesi hizo.
Max kwa ustadi mkubwa alifanikiwa kuingiza vijana wake hatari ndani ya Nchi, huku kwa makusudi makubwa akivujisha taarifa juu ya kuingia kwao hapa nchini.
Yeye na kundi lake walipofika Arusha walitafuta namna ya kufanya mauaji ya kutisha ili kuvifanya vichwa vya viongozi wa usalama viamini kuwa kulikuwa na mabaya yaliyokuwa yanakwenda kufanyika Arusha. Kwa utaalamu wa hali ya juu walifanikiwa kwenda hospitali ya umma mkoani na kufanya mauaji ambayo yamesababisha viongozi mbalimbali wa nchi hizi kutuma wapelelezi wao huko Arusha. Jacob toka Ofisi Fukuzi ni mmoja wao.
Hivyo wakati Jacob akiwa ofisini kwake muda mfupi tu mara baada ya kuwa amekabidhiwa kazi na bosi wake, Bi. Anita, ni wakati huo huo ambapo Max alikuwa ndani ya moja ya hoteli ya kifahari ndani ya jiji la Nairobi. Max alikuwa ameingia Nairobi kwa ndege ya asubuhi sana tokea Arusha ambako alikuwa amewaacha wenzie wakiwa wanapumzika na kufuatilia nyendo na mawasilino yoyote yaliyokuwa yakiingia na kutoka katika simu ya Edson Kinyaro.
Nairobi alikuwa anakutana na mzungu mmoja ambaye alikuwa amekuja kwa niaba ya wenzake. Yeye alikuwa amemwita Max ili kumkabidhi orodha na picha za wapelelezi ambao wazungu hao walitaka Max na kundi lake wawamalize.
“Naamini kazi yenu ya kuingia Arusha haikuwa ngumu sana. Na nina imani kwamba mmefanikiwa kuvifanya vyombo vya usalama kuwa na taarifa juu ya ujio wenu, kwani taarifa ya kutolewa vitisho kwa ule mkutano wa Amani ya Afrika Mashariki pale Arusha hata mimi nimezipata. Niliposikia hivyo nikajua kazi imeiva Tanzania.
Sikiliza Max, hizi hapa ni picha za wapelelezi ambao tungependa kusikia taarifa za vifo vyao. Ukiwamaliza hawa utakuwa umemaliza kazi yako katika hatua ya kwanza. Hapo utapokea kiasi cha pesa kama tulivyokubaliana katika mkataba wetu” Alisema mzungu huyo katika lugha ya kiingereza.
“Sawa, hesabu hii kazi imeshaisha. Jiandae kusikia vilio vikitokea huko Arusha” Alijigamba Max pasipo kujali chochote. Tamaa ya pesa ilikuwa imemjaa, mpaka kope zake zilionyesha hivyo.
* * *
Saa mbili asubuhi siku iliyofuata, yaani tarehe 18 Julai, 2009 ilimkuta Max akiwa tayari ndani ya Arusha. Tayari alikuwa ameshatoa vivuli vya kutosha vya zile picha alizokuwa amepewa na mmoja wa bosi wake kule Nairobi.
Wakati huu Max alikuwa ni mwenyekiti wa kikao kilichojumuisha vijana wake wa kazi.
“Kama mjuavyo kuwa kazi yetu ndiyo inatarajia kuanza leo hii. Bila shaka mara baada ya kusikia yote yale tuliyoyafanya pale hospitali ya mkoa na kwa yule jaji wa mahakama ya kimataifa, viongozi wengi wa usalama wa nchi hizi watakuwa wameshatuma wapelelezi wao wanaowategemea. Sasa, hapa nina picha za wapelelezi wote wanaotakiwa kuuawa. Nitawapa ninyi picha hizi halafu mtawapa vijana wetu.
Naomba mzingatie jambo moja, hapa tunakwenda kupambana na wapelelezi wanaotegemewa na nchi zao katika ukanda huu. Ni watu wenye mbinu zote za kipelelezi na ujasusi, hivyo yeyote atakayefanya mchezo nitammaliza hata kabla hajafikiwa na wapelelezi hao. Hili ni vema mkawaambia hata vijana wengine ili wawe makini” Max aliongea katika sauti ya utulivu kana kwamba alikuwa anaongoza ibada iliyojaa watakatifu.
Kikao hiki kiliwajumuisha watu ambao ni wataalamu watupu. Max kwa kutambua ugumu wa kazi aliyokuwa nayo alikuwa amechagua watu ambao kweli ni watu waliostahili kazi hii. Kiasi cha pesa alichokuwa amehidiwa kupewa kilitosheleza kabisa kuwalipa wataalamu hawa wa kutumia silaha na kupigana.
“Kwa wakati huu tutatawanyika na kwenda sehemu tulizopangiana, naomba kusiwe na makosa yoyote” Alipoongea maneno hayo wote walipiga makofi kuonyesha ushirikiano na umoja.
Ilikuwa ni saa nne kamili asubuhi ambapo kikao hicho kilifungwa na wote wakatawanyika.
* * *
Nusu saa baadaye baada ya kwisha kwa kikao cha Max na wenzie, ilimkuta mpelelezi Jacob Matata tayari akiwa miongoni mwa wasafiri waliokuwa wakisubiri muda wa safari katika kiwanja cha kimataifa cha ndege cha J.K.Nyerere zamani DIA, Dar es salaam. Alikuwa tayari kwa safari ya kutoka Dar kwenda Arusha. Moyoni alijua kuwa anaenda kama mpiganaji aliyetumwa na watanzania wote wapenda amani. Pia hakupinga wazo kuwa safari hii ilimaanisha kupata au kukosa, kuua au kuuawa.
* * *
Mchana wa siku hiyo ulimkuta tayari ameshaingia Arusha. Kuingia kwake alipanga akufanye siri. Hakupenda mtu yeyote ajue yuko wapi na anafanya nini. Hivyo alipotelemka tu toka ndani ya ndege alitembea taratibu huku akichunguza kama kulikuwa na macho yaliyokuwa yakimfuatilia.
Alikuwa amevaa miwani maalumu ya kijasusi ambayo humwezesha aliyeivaa kuweza kuona mbali sana. Miwani hii pia ina uwezo wa kuona mtu yeyote aliye na madhala kwa aliyeivaa. Ni miwani ya ajabu!
Alienda sehemu moja waliyokuwa wakiuza chakula na kuagiza kahawa. Yote hii ni katika hali ya kujipa nafasi ya kuweza kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akitarajia ujio wake. Alikunywa taratibu huku macho yake yakichunguza kila mtu katika sehemu hii ya uwanja wa ndege. Mpaka alipomaliza kinywaji chake hakuwa ameona yeyota wa kutilia mashaka.
Dakika chache baadaye zilimkuta amesimama kando ya taxi moja ya rangi ya bluu.
”Mzee naomba unipeleke Mlimani Hotel tafadhali” Alisema hivyo wakati tayari akiwa ameshakaa ndani ya gari. Dereva huyu aliyeonekana kuwa ni mtu wa makamo hakujibu kitu na badala yake aliwasha gari na kuliondoa kwa mwendo wa wastani.
Baridi ya wastani na ukungu mwepesi vilikuwa vimeipamba Arusha na kuifanya iwe katika hali yake ya asili. Waliposhika barabara ya Nyerere ndipo mpelelezi Jacob Matata akapata wazo la kuangalia kama kulikuwa na gari iliyokuwa inawafuatilia nyuma. Wakati wanafika mkabala na benki ya NBC tawi la Arusha ambalo liko jirani na Maktaba ya vitabu ya mkoa wa Arusha, upande wa mbele wa Polisi mesi, ndipo alipopata uhakika kuwa kulikuwa na gari lililokuwa likiwafuatilia.
Alitabasamu. Alifurahi kugundua kuwa kuna wajanja kama hao. Wakati bado anafikiria juu ya nani ambaye alikuwa amejua juu ya kuwasili kwake na kuamua kumfuatilia, jambo jingine lilimshangaza. Kilichomshangaza ni uamuzi wa dereva kuamua kuacha kuelekea Mlimani hoteli ambayo iko jirani na makutano ya barabara ya kijenge, Njiro, Philips na hii inayotokea mjini, badala yake dereva huyo akashika njia nyingine. Alipomtupia macho dereva huyo mshangao uliongezeka kwa Jacob baada ya kuonana na tabasamu alilokuwa usoni mwa dereva huyo.
Akiwa bado anashangaa tabasamu hilo na kujaribu kutafsiri kuwa lilikuwa limebeba ujumbe gani, mzee huyo alimshangaza zaidi pale alipoanza kucheka kwa sauti ya chini chini huku meno kadhaa ya kinywa chake yakionekana. “Samahani nitakuchelewesha kidogo” hatimaye mzee huyo alisema, baada ya kuona Jacob ameshangazwa na kitendo chake cha kuachana na safari yao na kuanza kuelekea upande mwingine.
Jacob aliangalia nyuma kuona kama lile gari alilohisi kuwa linawafuata kama lilikuwa bado linawafuta. Ndiyo! lilikuwa nyuma yao kwa tofauti ya magari mawili kati yao. Wakati Jacob anapapasa mfuko wake tayari kwa kutoa bastola yake, yule mzee naye aliongeza mwendo wa gari kwa ghafula!!
Alizipita gari kama tatu hivi kwa kasi na kukata kulia kuingia barabara ya benki kuu akawa kama anaelekea Central Arusha. Hapo aliongeza mwendo zaidi kabla ya kupunguza kwa ghafula na kuingia kulia, akapita ofisi za TRA Arusha kwa mwendo wa kasi, hadi pale walipokuwa wakitazamana na jengo la AICC, hapo aliingia kulia akawa anateremka kuelekea round about inayounganisha barabara inayotokea ilipo Meat King, Benki kuu na Arusha City Council. Hakuingia kwenye round about, akakunja kushoto, alipita mbele ya ofisi za mkuu wa mkoa kwa mwendo wa kasi, akateremka kwa kasi hadi alipofika mnara wa saa hapo akakunja kushoto kuchukua barabara inayoelekea Impala hotel. Aliyafanya yote hayo huku lile tabasamu lake likiwa bado limeupamba uso wake. Mpaka wakati huo Jacob hakuwa amefanikiwa kuelewa maana ya tabasamu hilo la utata.
Japo alionekana kuwa mtulivu zaidi kwenye kiti alichokuwa amekaa, lakini mambo kadhaa yalikuwa yakikitatiza kichwa cha Jacob Matata, tangu hapo alipokuwa ameshuka pale kiwanjani. Nadhani hata kama ungekuwa ni wewe, unaweza kuona kuwa mambo yanachanganya kweli. Kuja kwake Arusha aliifanya kuwa siri, sasa hawa waliokuwa wakilifuatilia gari hili alilopanda ni akina nani? Huyu dereva mzee kafanikiwa kuwakwepa, lakini hakuna aliyemwambia kuwa awakwepe na isitoshe amejuaje kuwa walikuwa wanawafuatilia wao? Hakuwa anajua Jacob ni nani. Kwa nini muda wote huu amekuwa akitabasamu pasipo kuongea neno lolote? Amweke kundi gani la wabaya au wema? Maswali yote hayo hakuyapatia majibu.
Walifika Mlimani hoteli saa sita na nusu mchana. Wakati dereva huyo akitafuta mahali pa kuegesha gari, Jacob akatumia fursa hiyo kumwangalia na kuitalii sura yake. Alianza kuamini kuwa yawezekana akawa si dereva kama madereva wengine.
Haikumchukua muda mrefu sana kuona tofauti, baada ya kuanza uchunguzi wake kwa mzee huyu, Jacob aligundua kuwa alikuwa amevaa sura ya bandia usoni.
ITAENDELEA!!

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...