Ads Here

Friday, September 27, 2019

HUJUMA

”Huwezi kuyaona, na wala hutakiwi kujua yako wapi, unachotakiwa kufanya wewe ni kuwasiliana na watu wako ili tufanye biashara, basi, hakuna kingine,” Shalabah alimueleza. Kisha akavuta mkoba wake na kufungua, akatoka kijitabu Fulani wakaandikiana mawasiliano yao na kisha wakaagana, kila mtu akachukua hamsini zake.
Shalabah akaikunja miguu yake na kuiweka kwa mtindo wa nne na kuagiza kinywaji kikali, alipoletewa alikuwa akinywa taratibu akisubiri miadi mingine, mara hii ya watu wake. Haikupita hata saa moja vijana watatu warefu, wembamba wakaingia na land cruiser pick up, wakateremka na kuungana naye katika kinywaji hicho.
CHAPISHO LA 02
“Mmekuja?” akawauliza wakati akiwaona.
“Ndio, mkuu, tumeitika wito,” wakajibu
“Sasa, nimeona kazi mliofanya, hongereni sana, lakini kama kuna jambo nataka kuwaambia ni kuimarisha ulinzi pale gahalani, silaha za safari hii hawa jamaa hawatakubali zipotee hivihivi lazima watakuja, hivyo muweke ulinzi wa kutosha kwa maana jamaa wako tayari na wanataka kuchukua mzigo wote kwa pesa iliyotakata sana. Mimi jioni ya leo nitakwenda kuonana na Top ili tuone mgao wenu mpaka hapa mlipofanikisha unakuwaje,” Shalabah alikuwa akiwaeleza wale vijana mpango ulivyo kwa ujumla.
Maharamia hawa walikuwa tayari kufanya biashara ya makombora hayo na kikundi kimoja kinachoendesha mapigano yasiyokoma huko katika jangwa la Pakistan mpaka Afghanistan, kutokana na kuishiwa na silaha nzito waliingia mkataba na maharamia hawa ili wawatafutie silaha nzito na zenye nguvu ili kuwaadabisha mahasimu wao, safari hii wakazipata. Pesa waliokubaliana kuyanunua ilikuwa ni pesa ambayo inaweza kulisha Tanzania nzima kwa miezi kumi na moja kwa milo mitano ya mlo kamili kwa kila mwananchi bila kujali mtoto au mtu mzima. Ilikuwa ni biashara haramu kuliko haramu yenyewe.
Mr SHALABAH aliendelea kuketi pale alipoketi mara baada ya kuiachana na wale vijana wake, akiwa katika kuburudika na kinywaji chake mara akajikuta hayupo peke yake katika meza hiyo, mbele yake kulikuwa na kijana mkakamavu aliyevalia suruali ya jeans na shati jepesi, usoni akiyaficha macho yake kwa miwani nyeusi iliyomkaa sawia.
“Biashara imeenda?”Shalabah akauliza.
“Kama kawaida, hakuna kinachoharibika hapa,” Yule kijana akajibu.
“Ok, mzigo uko kamili?” Shalabah akarusha swali lingine.
“Mzigo hauna shaka, uko sawa, mmetusaidia sana na mapinduzi yanaendelea,” Yule kijana akajibu. Akaisukuma briefcase ilikuwa chini kwa mguu wake wa kushoto, ikamgusa Shalabah, Shalabah akaitazama na kuiinua akaiweka mezani, akaifungua na kuchungulia kidogo, manoti ya dola za kimarekani yalikuwa yamejipanga kwa mtindo wa kupendeza, akatabasamu na kutikisa kichwa. Akaingiza mkono katika mkoba wake mdogo na kutoa kamashine kadogo, akabofya hapa na pale akatoa kijikaratasi Fulani na kukiweka saini kisha akampa Yule kijana na kuagana naye. Alipohakikisha amepotelea nje, akanyanyuka na kuibeba ile briefcase naye akaielekea gari yake aina ya Jaguar aliyoiacha kwenye maegesho na kuondoka kwa kasi katika hoteli hiyo.
§§§§§
Breki ya kwanza aliikanyaga mbele ya jumba kubwa la kifahari katika mtaa wa Wadada Jaziira, Ndani ya mji wa Mogadishu. Jumba hilo ambalo nyuma yake lilikuwa limepakana na bahari ya Indi lilikuwa limejitenga na majumba mengine, lilikuwa mbali kabisa na makazi. Shalabah alikunja kona na kulifikia geti kubwa la jumba hilo, na mara lile geti likafunguka lenyewe na kuruhusu Shalabah aingie, akakanyaga mafuta kuifuata barabara inayoelekea katika jumba hilo ambalo lilijengwa umbali wa kilomita moja kutoka getini, aliegesha gari yake katika eneo maalumu, akashuka na ile briefcase mkononi na kuelekea mlango mkubwa wa jumba hilo. Vijana wawili wenye bunduki kubwa zenye nguvu walikuwa wamesimama katika mlango huo, mmoja huku na mwingine kule, walimkagua Shalabah na kuhakikisha hana silaha yoyote mwilini mwake, wakamruhusu kuingia ndani ya jumba hilo.
Jumba lote lilikuwa kimya kabisa, ni viatu vya Shalabah tu vilivyokuwa vikisikika wakati huo, akapanda ngazi kuelekea juu mpaka ghorofa ya kwanza, akapita tena katika korido ndefu iliyopambwa kwa sakafu na kuta za mbao safi ambazo polishi iliyopakwa na kung’aa sawia ilikufanya mpitaji ujione pande zote nne. Baada ya milango kama sita hivi, Shalabah alifika katika mlango wa saba akageuka na kuutazama, kulikuwa na kidubwasha chenye tarakimu tisa, akabofya tarakimu hizo kwa mtindo anaoujua yeye na mara ule mlango ukafunguka, Shalabah akaingia ndani ya kijichumba hicho kidogo na ule mlango ukajifunga, kisha kile chumba kikaanza kuteremka chini, kikaiacha ile mandhari ya mbao na kubaki kioo tupu, Shalabah aliweza kuona samaki aina mbalimbali na mandhari nzuri ya chini ya bahari, mara kile chombo kikaingia tena katika mandhari nyingine ya mbao zenye kung’aa kama zile za mwanzo, mara ikasikika sauti Fulani ikabip, ule mlango ukafunguka na Shalabah akateremka na kuifuata njia nyingiine ndefu mbele kulikuwa na mlango mwingine, ukafunguka kabla hata ya kuugusa, akaingia na kujikuta kwenye sebule pana yenye vitu vya thamani sana.
“Karibu Mr Shalabah,” sauti ilimkaribisha. Shalabah akaketi katika moja ya viti vilivyomo katika sebule hiyo. Mbele yake katika ukuta kukajitokeza luninga kubwa ‘flat’ na hapo aliweza kumuona Yule anayeongea naye.
“Ndiyo Mr. Shalabah, nipe ripoti kwa ujumla,” Yule mtu kwenye ile screen alimwambia Shalabah.
Shalabah alitoa taarifa kamili ya mchakato mzima wa utekaji wa manowari ya kijeshi iliyotoka Tanzania, pia akamweleza kuhusu pesa aliyolipwa na Yule kijana kwa biashara nyingine waliyokuwa wameifanya siku chache za nyuma.
“Vizuri sana,” Yule bwana kwenye ile luninga akajibu, kisha akaendelea, “Sasa kuna mpango gani kuhusu hizi silaha za sasa?” akuliza.
“Kwanza wale jamaa walitaka makombora lakini hawakusema idadi, sisi tumepata makombora makubwa kumi na mbili na silaha nyingine nyingi za kufaa,” Shalabah alieleza.
“Ok, hakikisha kila kitu kinakwenda sawa, imarisha ulinzi ijapokuwa naamini hakuna wa kutuumiza kichwa kwani kwa taarifa ambazo ninazo mpelelezi mkorofi wa Tanzania hayupo kazini kwa kipindi kirefu na nafasi yake imechukuliwa na mwingine, hakikisha kila mtu anayekuja kuhusiana nah ii shughuli unamuua, hakuna kumpa mtu nafasi hata ya robo sekunde, weka watu kila mahali, kila sehemu nyeti hakikisha umeweka kinasa sauti kilicho hai na Yule mdunguaji niliyekwambia umkodi ulimpata?” Yule bwana kwenye luninga alijaribu kupanga na kuuliza.
“Bila shaka mzee, nimempata na leo jioni nitaingia naye mkataba,” Shalabah akajibu.
“Sasa umwambie mkataba wetu utakwisha pale tu jamaa hawa watakapochukua mzigo wao, na hao mateka hakikisha tunawauza kwa vikundi vya ugaidi kwani nao ni silaha nzuri sana,” yule mtu kwenye luninga alimaliza na kisha ile luninga ikadidimia chini, pale ilipokuwapo pakatoakea picha kubwa ya mwanamke aliyelala uchi.
Mlio wa bip ukasikika, Shalabah akainuka na kuiacha ile briefcase palepale akatoka na kuingia katika kijichumba kile alichotokea mwanzo, kikampandisha na kumleta juu kabisa, akashuka na kuondoka zake huku akiliacha lile jumba nyuma yake likifanya mandhari safi inayolipamba jiji la Mogadishu.
Shalabah alikanyaga mafuta mpaka eneo linguine kabisa la mji, hapo palikuwa na jengo kama shule kubwa, Shalabaha akaingia na kupita moja kwa moja kwenye jengo linguine lililokuwa limejengwa ndani yake.
“Karibu sana bwana mkubwa, tukusaidie nini?” mlinzi wa eneo hilo aliuliza kwa sauti ya majigambo huku akimtunishia kifua Shalabah.
“Nahitaji kumuona bosi wako,” Shalabah akajibu.
“Unaitwa nani na umetoka wapi?” Yule mlinzi akauliza.
“Shalabah, kutoka Uranus,” akajibu. Yule mlinzi akainua simu na kupiga sehemu fulani, kisha akaongea maneno machache na alipoirudisha simu hiyo mahala pake, akamruhusu Yule bwana kuingia ndani. Shalabah alijikuta kwenye uwa mkubwa uliokuwa na watoto wengi waliokuwa katika mafunzo makali ya karate na kungfu, mkufunzi wao aliyekuwa mbele kabisa alionekana kuwa stadi sana kwa minyumbuliko aliyokuwa akifanya akiwaelekeza jinsi ya kukunja mikono na jinsi ya kusimama kimapambano.
Shalabah alipitishwa kwenye ujia mrefu mpaka katika mlango mmojawapo kati ya mingi, akaingizwa ndani na kuketi katika sebule kubwa lenye nakshi za kuvutia, zuria la gharama liliificha sakafu safi ya terrazzo, Shalabah alikuwa akiitalii sebule hiyo kubwa ya kuvutia iliyokosa kitu kimoja tu, muziki, muziki mororo ambao ungemfanya aliyeketi katika moja ya matandiko hayo ama achezeshe mguu au kichwa kufuatisha midundo ya muziki huo. Shalabah akiwa katika mawazo hayo mara akasikia mlango ukifungwa nyuma yake, akageuka lakini hakumuona mtu, aliporudisha uso wake mbele alikutana na mtu aliyekwishaketi tayari katika tandiko moja wapo mbele yake. Mtu aliyevalia juba la kibuluu lililoficha mwili wote na kuaacha macho mawili tu yaliyokuwa yakionekana kwa taabu kidogo. Shalabah hakujua kama mtu huyo ni mwanamke ama mwanaume kutokana na vile alivyovaa vazi lake hilo.
“Mr Kalabah, karibu sana katika himaya yangu,” Yule mtu alimkaribisha, Kalabah alimtambua kuwa ni mwanamke kutokana na sauti yake.
“Nimekwishakaribia, shukrani,” kalabah alishukuru.
“Tusipoteze muda, niambie shida yako,” Yule mwanamke alimweleza.
“Bimekuja kutoka Uranus, nina shida ya kikazi kama ofisi ilivyonituma,” Shalabah akiwa aneleza lililomleta, akaktishwa na sauti ya nhuyo mwanamke.
“Kazi au biashara?” akauliza.
“Si biashara kwa kuwa hakuna tunachotaka kukuuzia, ila kazi kwa kuwa tunataka ututekelezee jambo Fulani,” Shalabah akaeleza.
“Ok, linahusu damu ya mwanadamu?” Yule mwanamke akauliza.
“Ndiyo, litahusisha,” Shalabah akajibu.
“Sikila Mr. Shalabah, kwa hilo unalotaka tuongee hapa si mahali pake, nitakuelekeza wapi tuonane, hatuwezi kufanya biashara ya damu katika kasri hili tukufu, kasri la marehemu baba yangu alilotumia kuabudu, wewe nenda na mimi nitakujulisha wapi tuonane,” Yule mwanamke akamaliza kuzungumza na kuinuka kutoka pale alipokuwa ameketi akatokomea katika mlango mmoja wapo. Shalabah akainuka tayari kutoka ndani ya jumba lile, msichana mrembo wa uso alikuwa tayari kumwongoza kumtoa nje ya kasri hilo.
Shalabah alitolewa nje ya jengo lile kwa kupitia njia ileile lakini mara hii ali[pofika kwenye ule uwa akasimama na kushangaa anachokiona, mara ya kwanza alikuta watoto wakifanya mafunzo ya kungfu na karate, lakini mara hii alikuta uwa wote umeota nyasi na wanyama kama mbuzi walikuwa wakiburudika, alishindwa kuuliza akaamua kupitiliza mpaka nje ambako aliagana na Yule msichana akalielekea gari lake. Alipoketi nyuma ya usukani ndipo alipoiona kadi ndogo nyeupe ikining’inia katika swichi ya kuwashia vifuta maji (wipers) vya gari hiyo, akainyakuwa na kuisoma.
‘…Dar es salaam Club, saa 3:00 usiku…’
Akainyakuwa na kuitia mfuko wa shati, kisha akawasha gari na kuondoka zake.
SHUGHULI NDIYO HIYO... MAHARAMIA WAMETEKA MANOWARI YA JW, JE NINI KITAFANYIKA .... WAKATI HUOHUO MAHARAMIA NAO WANAJIPANGA KWANINI?

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...