Ads Here

Friday, September 27, 2019

RIWAYA: HUJUMA

SEHEMU YA III
‘…Dar es salaam Club, saa 3:00 usiku…’
Akainyakuwa na kuitia mfuko wa shati, kisha akawasha gari na kuondoka zake.
2
Makao makuu ya jwtz
Lugalo – dar es salaam
TAARIFA za kupotea kwa manowari ya jeshi la Tanzania na wapiganaji wake zilifika katika makao makuu ya jeshi hilo pale Lugalo mnamo majira ya saa tatu ausbuhi muda ambao manowari ile ilitakiwa kuwa imefika katika moja ya vituo vyake kabla ya kuwasili katika bahari ya Caspian siku mbili zinazofuata. Jeshi la Urusi lilipowasiliana na lile la Tanzania ilionekana wzi kuwa manowari hiyo imepotelea katika bahari ya Indi usiku uliotangulia, kwani kila walipojaribu kuitafuta kwa vifaa vya kisasa walishinda kabisa kuiona ilipo lakini waliweza kuona ilipoishia safari yake.
Wakipiga picha ya eneo hilo wanakuta ilikuwa sehemu za Somalia ijapokuwa ilikuwa katika maji makubwa, maji ya kimataifa.
Mkuu wa majeshi, brigedia jenerali Kamsumi alikuwa ameketi na viongozi wake wa ngazi ya juu kabisa jeshini wakijaribu kujadili juu ya upotevu wa manowari hiyo. Ulikuwa ni mkutano mzito ambao kila mshiriki alionekana kushikwa na jazba au hasira.
“Hao ni maharamia tu, si wengine, siku hizi wamekuwa wakiteka meli nyingi bila kujali sheria za kimataifa kuwa meli hizo ziko katika maji ya kimataifa, kwa nini tunawadekeza?” alilalama mmoja wa washiriki aliyekuwa katika jopo hilo.
“Meli sio tatizo, lakini vipi kuhusu makombora hayo ambayo gharama tu ya kuyatengeneza ilikuwa ni kubwa ijapokuwa tumepata ufadhili wa asilimia Fulani ya Warusi, tukiyaacha hawa jamaa si watatugeuka wenyewe?” Mjumbe mwingine alieleza.
“Hivyo vyote havina maana, wapiganaji wetu, watoto wetu wametekwa au kupotea pamoja na manowari hiyo kwa nini tuvumilie? Tuna makomandoo hapa tutume japo wawili tu wakaitafute hiyo meli kisha tuikomboe,” mjumbe wa tatu alikuwa akiongea mpaka anatoa machozi.
Baada ya majadiliano marefu na yaliyokuwa hayana mwisho, muada ulifika wa kufanya video conference na amiri jeshi mkuu. Luninga iliyokuwa ukutani ikachukua uhai na moja kwa moja mbele yao akainekana mheshimiwa Rais. Mkuu wa majeshi akaeleza kwa kifupi waliyojadiliana wajumbe katika kikao kile.
“Sikilizeni, hatuwezi kuvumilia wala kuwapa nafasi, ile ni pesa ya kodi za Watanzania, kwa nini ipotee hivihivi? Isitoshe kuna watoto wetu, vijana wetu na wapiganaji wetu, lazima waokolewe kwa gharama yeyote,” amiri jeshi mkuu aliongea kwa ukali sana, “Ninyi mna kitengo cha upelelezi ndani ya JW, haya mara moja chagueni mtu au watu wakafanye kazi hiyo, nitahitaji ripoti haraka,” mwisho wa maneno hayo ile luninga ikazimika. Kila mshiriki alishusha pumzi ndefu. Ilikuwa ni sentensi ndefu kidogo iliyowatetemesha wakuu hao wa jeshi waliokuwa wakibishana bila kupata muafaka katika lipi la kufanya. Kutokana na kauli ya aamiri jeshi mkuu, hakukuwa na mjadala mwingine kilichoangaliwa kilikuwa ni nani apewe kazi hiyo.
“Lakini jamani ee, tuiangalie hii kazi kwa ugumu na upana wake,” kiongozi mmoja alisema.
“Yeah ni kweli kuliko kudharau na kupeleka mtu ambaye atafika na kushindwa kufanya lolote. Nani tumtume akafanye kazi hiyo, kazi yan hatari kuliko hatari mwenyewe. Chekecha chekecha ikapita, Jamil Semindu, komandoo aliyemeliza mafunzo yake siku si nyingi nchini Cuba, jina lake lilipitishwa tayari kwa kazi hiyo. Mchana wa siku hiyo kijana huyo aliitwa makao makuu ya jeshi kutoka kambi ya Lugalo kule Mwenge. Naye hakukataa wito bali aliamini msemo wa wahenga, ;usikatae wito kataa neno’.
Majira ya saa nane mchana, Jamil Semindu alikuwa amesimama wima kiukakamavu mbele ya mkuu wa majeshi. Hakuwa peke yake, pembeni yake kulikuwa na mtu mwingine wa makamo, aliyavalia nguo nadhifu ya kijeshi.
“Jamil Semindu, Gwamaka Mwakajinga, tunatambua umuhimu na mchango wa kazi yenu katika jeshi letu tukufu la wananchi wa Tanzania. Nimekuiteni hapa kuwapa kazi maalum ambayo inatakiwa kuanzwa mara moja, kama mnavyojua au milivyosikia, manowari yetu ya jeshi la Tanzania, Kirov Class, ndani yake ikiwa na wapiganaji ishirini na tano pamoja na makombora kumi na mbili ya R-36 imepotea katika maji ya kimataifa huko Somalia, inahisiwa kuwa huenda ikawa imetekwa na maharamia kama iloivyotokea kwa meli zingine za mizigo. Tunawatuma muende mkafanye kazi, kwanza mkawaokoe wapiganaji wetu, pili mkaokoe makaombora yetu, tatu mkailete na meli yenyewe, mambo yote yamekwisha andaliwa mkitoka hapa tu mtaelezwa cha kufanya,” alimaliza mkuu jeshi. Wale wanajeshi wawili wakapiga salute na kisha kutoka nje ya ofisi hiyo.
Gwamaka Mwakajinga alikuwa mpelelezi wa kijeshi aliyeaminika sana hasa kwa kuzisoma nyanyo za adui, na kujua wapi alipo. Kijana huyu ndiye aliyewaongoza wenzake katika vita ya ukombozi huko visiwa vya Komoro, vita ya kumng’oa madarakani aliyekuwa rais wan chi hiyo. Alishiriki pia kupeleleza vizuri sana makazi ya waasi wa M23 pamoja na kujua maisha yao ya kila siku, mwisho wa siku aliwapa ramani yote majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na Tanzania na kuwafutilia mbali waasi hao. Jopo lililokaa kuchagua wawili hao liliangalia mambo mengi na tofautitofauti.
Gwamaka na Jamil wakapeana mikono na kusalimiana wakati wakiwa nje ya jengo hilo, kisha wote wawili wakaelekea katika jengo linguine kama walivyoongozwa.
“Unaonaje Meja, hawa vijana watawaweza wale maharamia wanaokunywa damu?” Luteni kanali Gogo alimuuliza mwenzake aliyekuwa naye, kapteni Kamazima.
“Wataweza tu, tuweke imani,” Meja Kamazima alimjibu.
“Maana wale maharamia kuwapata ni kazi, nao pia wamejikamilisha kwa silaha na upiganaji wa silaha,” Luteni Kanali Gogo alionesha waziwazi wasiwasi wake katika hili.
“Wataweza tu usihofu,” Meje Kamazima alimjibu na kumtia moyo mwenzake.
Taratibu zote zilikamilishwa za safari za hao jamaa, na siku iliyofuata kwa kutumia ndege ya shirika la ndege la Ethiopia waliondoka Tanzania kuelekea Somalia kupitia Addis Ababa.
“Sijacheza michezo hii siku nyingia sana,” Jamil alimwambia Gwamaka.
“Michezo midogo sana hii, nilikuwa Kivu juzijuzi tu kuwasaka M23 hivyo bado damu ya moto,” akazungumza Gwamaka. Walibadilishana mawazo wakiwa katika ndege hiyo safarini kuelekea Mogadishu.
“Sasa sikia Jamil, unajua hawa jamaa ni wajanja sana, kwa vyovyote lazima wanajua kama tunakwenda, tukifika naomba tushuke kila mtu kivyake na tusijuane isipokuwa tuwasiliane kwa simu tu kila mtu atakapofikia,” Gwamaka alijaribu kupanga mpango.
“No, tufikie hotel moja lakini tutofautishe vyumba kwa umbali mrefu kama kuna ghorofa basi mmoja ya juu mwingine ya chini,” Jamil naye akatoa pemdekezo ambalo lilikubaliwa na wote.
“Tutafanyaje operesheni yetu?” Jamil akauliza.
“Kutokana na kazi zetu, mi nitakuwa nafanya uchunguzi nakupa information na wewe unakwenda kumaliza kazi maana we ni jeshi la mtu mmoja,” wote wakacheka na kugonga viganja vyao.
RAMADA PLAZA HOTEL
Ramada plaza hoteli, ni hotel tulivu iliyo jirani na bahari katika jiji la Mogadishu, ikitazamana na bandari ya zamani ya jiji hilo. Mandhari safi, chakula na mazingira ya kuvutia viliwafanya wapiganaji hawa kuvutiwa na mahali hapo.
Alikuwa Gwamaka wa kwanza kuingia katika hotel hiyo, akapanga chumba ghorofa ya tatu juu. Baadae jamil nae akafika na kuchukua ghorofa ya chini kabisa, wakiwa tayari kikazi na wamekamilika.
Kutoka ghorofa ya tatu Gwamaka aliweza kutumia darubini yake kuangalia upande wa baharini kila baada ya nusu saa na kuandika kwenye kidaftari chake mambo anayoyajua mwenyewe. Jioni ya siku hiyo wakiwa chakulani walibadilishana mawazo hili na lile na kupanga nini cha kufanya.
§§§§§
DAR ES SALAAM CLUB
SHALABAH aliegesha gari yake katika maegesho ya club hiyo ya usiku, akateremka na kuufunga mlango nyuma yake. Kisha kwa hatua za taratibu aliuendea mlango mkubwa. Kwa upande wa nje zaidi ya walinzi walioonekana kuangalia usalama wa mali za wateja, hakukuwa na vurugu wala hakukusikika kelele yoyote ya kitu chochote, mtaa ulikuwa kimya kabisa. ni wale tu waliokuwa hawafuati sawasawa misingi ya dini yao ndiyo waliokusanyika katika klabu hiyo pamoja na wageni kutoka Katika nchi za pembezoni na zile za mbali.
Shalabah alizipanda ngazi na alipofika katika mlango wa kuingilia alisimamishwa na akatakiwa kusalimisha kama ana aina yoyote ya silaha, alikuwa na bastola moja na kisu cha kukunja, akaviacha na kuandikisha, akapewa namba na kuingia ndani.
Tofauti na nje, ndani ya klabu hiyo kulikua na kila aina ya starehe, muziki laini ulikuwepo na wale waliopenda disco walitakiwa kuteremka chini kabisa. watu walikula na kunywa wakifurahia maisha. Shalabah alijipenyeza taratibu katika makundi ya watu mpaka akaifikia kaunta kubwa.
“Nikusaidie nini?” akauliza mtu aliyekuwa kaunta. Shalabah hakujibu isipokuwa alitoa sigara na kumuonesha, kisha yule jamaa akatoa kiberiti na kukiwasha lakini hakuiwasha ile sigara. Sekunde chache tu mwanadada mrembo aliyekuwa na nywele mpaka kiunoni alimjia Shalabah na kumshika begani. Shalabah akamfuata. Wakapenya penya katika makundi ya watu, wakapita nyuma ya jukwaa la wacheza uchi wakaingia kwenye pazia la kumetameta, ndani ya mlango mkubwa na mzito wa kioo, hakukuwa na kelele yoyote, palikuwa kama nyumbani, huko kulikuwa na vyumba vingi sana.
809, yule mwanadada akasimama na kubofya kitufe Fulani, mlango ukafunguka, wakaingia. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na chumba kimoja kidogo na mwanadada mrefu aliyekuwa na upara kichwani mwake huku akivuta mtemba kinywani mwake alikuwa amekunja nne kwenye sofa moja pana na kuiachia nguo yake yenye mpasuo mrefu kumwagika kwa chini na kuruhusu mapaja yake laini kuonekana kwa ukamilifu.
“Karibu Kijana,” yule mwanamke akamkaribisha.
“Asante sana,” Shalabah akajibu.
“Haya tuna dakika tano tu za kuzungumza, nipe mzigo, nikupe kipimo,” yule mwanamke mwenye upara akamwambia Shalabah.
“Nafikiri unatufahamu, sasa tuna biashara nzito sana ya kufanya, ijapokuwa hatuna hofu na usalama kutokana na biashara zetu zilizopita, ila hii tumetahadharishwa sana, kuna watu tunatakiwa kuwaondoa haraka iwezekanavyo lakini pia tunahitaji usaidizi wa kiteknolojia katia kuyatambu makombora kumi na mbili tuliyoyateka,” Shalabah alieleza.
“Ha ha ha ha nyie watu mna biashara za hatari sana, kwa kuwa tuliingia mkataba huo tangu mwanzo na tajiri wenu hamna tabu, haya kazi ya kwanza itafanyika, nipe picha za hao watu na wapi wamefikia, kuwatungua si tatizo, kisha tutaliona la pili,” yule mwanamke mwenye upara akaeleza. Shalabah akatoa Ipad yake na kuparazaparaza vidole vyake kwenye kioo cha chombo hicho, kisha akamkabidhi yule mwanamke. Akachukua na kutazama, naye akaparaza hapa na pale na zile picha zikahamia kwenye simu yake ya kisasa kwa njia ya Bluetooth.
“Ok Mr. kila kichwa dola 1000 za kimarekani, nimemaliza, fanya mchakato kama tunavyofanya kila wakati,” yule mwanamke akanyanyuka na vazi lake likamfunika vyema, akafungua mlango wa nyuma yake na kutokomea. Shalabah alitoka ndani ya chumba kile na kutembea taratibu kurudi ukumbini, kisha akatoka nje ya klabu ile.
§§§§§
Ndani ya bahari ya Indi katika bandari ya zamani ya Mogadishu, maharamia wateka meli walikuwa katika ulinzi wa aina yake. Walionekana ni watu masikini kimavazi lakini ukiwatazama silaha walizobeba mikononi mwao utakubali tu. Wapo waliokuwa juu muda wote wakitazama usalama kwa kujifanya wana shughuli mbalimbali. Na daima walikuwa wakifuatilia sana nyendo za wageni wanaoingia Somalia hasa wale kutoka nchi za maghalibi kwa maana walikwishateka meli kadhaa za mataifa hayo na kuwaweka mateka wanajeshi wao. Hata zile nchi zilipojaribu kutaka kuwapata watu hao ilikuwa ngumu kutokana na nchi ya Somalia kutokuwa na serikali ambayo unaweza ukafanya mazungumzo nao.
Wapiga mbizi kadhaa walikuwa ndani ya maji wakikagua makombora hayo, upande wa wale wanaouza ambao ni hao maharamia na wale wanaouziwa wapiganaji waasi kutoka huko Pakistani na Afghanistani, walikuja na wataalamu wao na wakati huo maharamia hao nao walikuwa na mtaalamu wao wa silaha, mwanamke yule mwenye upara. Ukaguzi ulifanyika chini ya maji kwa muda takribani wa dakika thelethini, kisha wapiga mbizi hao wakatokea ndani kwa ndani na kuingia katika chumba kilichojaa maji ambacho kuna ngazi unapanda na kutokea chumba cha juu kisicho na maji. Hapo wakavua mitambo yao walioibeba migongoni na kubaki katika nguo zao za kawaida. Kisha wakafuatana kutoka na kuingia katika gari iliyoandaliwa wakaelekea mjini.
Kepteni Gwamaka Mwakajinga akashusa darubini yake kutoka katika uso wake akaichia ining’inie kifuani.
“Wametoka,” Gwamaka akawasiliana na Jamil aliyekuwa kwenye gari nyingine.
“Wasindikize, unambie wanapoishia,” Jamil akamwambia Gwamaka. Kwa mwendo wa taratibu Gwamaka akaingiza gari barabarani na kuendessha kuelekea kule ambako gari ile ilikwenda. Alihakikisha haipotezi kabisa gari hiyo katika macho yake.
Aliendelea kuwafuata akiwa peke yake ndani ya gari.
“Gwamaka, kuna gari imenipita kasi sana hapa hebu iwekee tahadhari,” Jamil aliwasiliana na Gwamaka wakati gari hyo aliyoisema ikiwa mbele yake kama mita kumi tu. Walipoiacha barabara ya Corso Somalia na kuupita mzunguko kisha kuikamata barabara ya Jidka Jannaral Daud ndipo komandoo Jamil alipoona hila ya watu hao, akajua wazi kuwa wako matatani na hana budi kumsaidia mwenzake aliyekuwa mbele.
“Nimeiona,” akajibu.
“Kaa tayari, jamaa wameandaa silaha nahisi wanataka kufanya shambulizi la ghafla,” Komandoo Jamil alimwambia Gwamaka.
“Natafuta mbinu ya kufanya,” Gwamaka akamwambia Jamil.
Haikupita sekunde thelathini, wakati wanakaribia kabisa shule ya sekondari ya Jan Daud, ile gari nyuma ya Gwamaka ikaovateki ghafla na kukaa upande wake wa kushoto, Gwamaka akawa tayari amekwishaiona, akaipa sekunde mbili ilipokuwa tayari inakaribia nusu ya gari yake kuovateki, nae akaitoa gari yake kushoto, na kusababisha dereva wa wale jamaa kuyumba, ile gari ikagonga nguzo ya umeme, cheche zikawaka na transifoma la jirani likalipuka.
“Usisimame, wafuate,” Komandoo Jamil akamwambia Gwamaka kwa simu yake ya upepo yeye akiwa katika gari iliyokuwa nyuma yao umbali wa mita kama hamsini hivi, aliishuhudia ile gari ikigonga nguzo na ule moto wa umeme uliolipuka ukafanya gari ile kushika moto. Jamil alishuhudia watu wale walivyokuwa wakijaribu kutokea madirishani.
“Safi sana Gwamaka!!!!” Komandoo Jamil aliikubali mbinu iliyofanywa na Gwamaka, akaongeza mwendo na kuzipita gari mbili zilizo katikati yake. Akapunguza mwendo na kushuhudia wawili wakiungua vibaya kwa kushindwa kutoka ndani ya gari, na mmoja akiwa ndiye anajinasua dirishani. Komandoo Jamil, akaegesha gari pembeni na kuteremka kwa minajiri ya kutoa msaada, akamuendea yule wa dirishani na kumnasua katika kioo, akambeba na kumtia kwenye gari yake.
INAENDELEA...

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...