Ads Here

Saturday, September 21, 2019

Mtego Mahsusi

By Patrich Massawe
Mtego Mahususi
Na Patrick J. Massawe

LUTENI Jonas Gumbo, kijana msomi na Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, bado ana kiu kubwa ya kujiendeleza kimasomo zaidi. Anaomba maombi ya kwenda kusomea Shahada ya Pili ya Uhusiano wa Kimataifa nchini Uingereza ambapo anakubaliwa bila kipingamizi chochote. Lakini upande wa pili, kuna siri nzito iliyojichimbia nyuma ya mapazia. Kuna Kundi moja hatari la Kijasusi linalojiita ‘Nge Wekundu,’ ambalo kwa njia moja ama nyingine lilimsaidia Jonas kuipata nafasi hiyo ya kusoma nje ya nchi, hivyo linamhitaji kwa kazi moja muhimu sana. Limwekea mtego mahususi utakaoweza kumnasa ili akubaliane na matakwa yao waliyopanga. Je, ni kazi gani hiyo muhimu? Na watafanikiwa kumpata mpiganaji huyo mahiri? Fuatilia hadithi hii ya kusisimua yenye misukosuko mingi…

GARI moja la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi, pia likiwasha taa za tahadhari na kupiga honi mfululizo, lilisimamishwa nje ya Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam, kunako majira ya saa nane za mchana. Vumbi zito lilitimka na kuwa na patashika nzito! Askari Polisi wa Kikosi maalumu, waliokuwa na bunduki zao,  walishuka harakaharaka kulizunguka gari hilo, wakiwa wameziweka silaha hizo tayari kwa kuzitumia endepo ingetokea rabsha ya aina yoyote!
Ndani ya gari hilo la polisi, alikuwepo mtuhumiwa tishio na hatari, ambaye walimshusha haraka na kumsindikiza katika ulinzi mkali, na hatimaye akaingizwa ndani ya jengo lla Kituo Kikuu cha Kati. Mtuhumiwa huyo alifikia katika ofisi maalumu ya Idara ya Upelelezi, akionekana kama ni bidhaa adimu mbele ya maafisa wale wa polisi, ambao muda wote walikuwa hawaamini kile kilichotokea ndani ya saa arobaini na nane zilizopita!
Huko nje waliacha umati mkubwa wa watu waliokuwa wamejazana kulizunguka jengo lile la kituo, kushuhudia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Umati ule ulipenda kumwona, alikuwa ni mtu wa aina gani, aliyekuwa ameamua kujitoa mhanga kwa kuenda kitendo cha ajabu ndani ya nchi iliyojaa amani ya kutosha! Ni jambo ambalo lilikuwa halijazoeleka hapa nchini Tanzania, zaidi ya kutokea katika nchi za wenzetu zenye vurugu za kiutawala na uchu wa madaraka!
Mtu huyo alikuwa ni mtuhumiwa hatari aliyehusishwa na tuhuma za ujasusi, kiasi cha kulifanya jiji zima la Dar es Salaam livume kwa mtikisiko wa milipuko ya mabomu yaliyoacha baadhi mya watu wakiwa majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali. Ni milipuko iliyokuwa ikirindima tokea usiku wa kuamkia jana yake na kuwaweka polisi na watu wa Idara ya Usalama wa Taifa katika wakati mgumu na kutojua kilichokuwa kinaendelea. Ni nani aliyekuwa anaratibu mipango ile?
Hawakujua!
Ndiyo, alikuwa ni kijana mtanashati, msomi, na Ofisa wa Jeshi, Luteni Jonas Gumbo, mpiganaji mahiri aliyehitimu katika medani ya kivita. Baada ya kuingizwa ndani ya chumba cha upelelezi, alihojiwa kwa muda mrefu ili atoe maelezo ya kina juu ya kuhusika kwake na tuhuma zile za kijasusi zinazomkabili. Alipomaliza kuhojiwa, ndipo alipopelekwa ndani ya chumba maalumu cha mahabusu, akisubiri hatua zinazofuata. Ukweli ni kwamba Jonas alibaki akiwa amechanganyikiwa baada ya kukutwa na dhahama ile ya kujitakia kwa kujiunga na kundi la kijasusi kwa minajili ya kupatiwa malipo ya ziada!
Luteni Jonas alikuwa ni Ofisa wa Jeshi aliyekuwa anapata mshahara wa kumtosha yeye na familia yake. Lakini akajikuta akishawishiwa na kulazimika kujiunga na kundi hilo, ingawa hakupenda. Akiwa amejiegemeza katika ukuta wa chumba hicho cha mahabusu, alikuwa akimlaani mwanadada wa kizungu, Clara McCauley, aliyemwingiza katika mtego ule, bila kumsahau, Burhan Karim, mtu aliyekuwa akishirikiana naye katika kazi zile za kijasusi. Ni mtu ambaye asingemsahau katika maisha yake!
Luteni Jonas alichokumbuka mara ya mwisho, ni kwamba baada ya purukushani iliyotokea kule Uwanja wa Ndege mwa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati wakirushiana risasi na askari wa usalama, ni kwamba alimwona mshirika mwenzake, Jasusi, Burhan Karim, akiwa amepanda pikipiki kubwa, akilifukuza lile gari la polisi alilokuwa amepanda, ili aweze kulilipua kwa bomu alilokuwa nalo mkononi. Nia yake ilikuwa ni kuwalipua wote kwa madhumuni ya kupoteza ushahidi, lakini alichoshuhudia baada ya kipindi kifupi tu, ni kwamba Burhan alianguka kutoka juu ya pikipiki yake na kufikia chini katika lami! Alilipuliwa na lile bomu kiasi cha kutawanywa vipandevipande vya nyama na kutawanyika katika eneo lote. Hivyo hakuweza kumwona tena hadi alipofikishwa kwenye Kituo cha Polisi cha Kati!
Hakuishia hapo, Jonas alimkumbuka mke wake, Consolata, na mwanawe, Kelvin. Alijua kuwa asingewaona tena kwa tuhuma zile zinazomkabili, kwani kifo cha kupigwa risasi kama msaliti kilikuwa kinamsubiri. Majuto yaliendelea kumwandama huku akiwapiga baadhi ya mbu waliokuwa wakimzunguka na kufanya sherehe ya damu katika mwili wake. Akasonya na kubaki amekaa pale sakafuni mawazo yakiwa mbali!
Lakini ukweli unabaki kwamba, kujiunga kwake na kundi lile la kijasusi la ‘Nge Wekundu,’ zinamhusisha mtu mmoja tu, Burhan Karim, chotara wa kizungu, aliyekuwa mwakilishi wa kundi hilo katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki. Historia ilianza yapata miaka hamsini iliyopita kabla ya  Vuguvugu la Mapinduzi ya Utawala wa Kisultani, huko Unguja, kunako mwaka 1964. Huko ndipo lilipotokea chimbuko la jasusi huyo hatari, Burhan Karim Kizango!

          ********
Ulikuwa  ni usiku wa hofu!
Ni usiku wa manane, ambapo makelele ya kuomba msaada yaliweza kusikika kutoka kwa wakazi wanaoishi katika viunga vyote vya mji wa Unguja. Umeme ulikuwa umekatika na kufanya kote kuwa na giza la kutisha, pia, kelele hizo zilizoambatana na vishindo vya watu, na baadhi ya askari wa utawala wa Kisultani, waliokuwa wakikimbia katika kuokoa maisha yao yaliyokuwa hatarini katika maangamizi makubwa ya umwagaji damu.
Katika purukushani ile ya usiku wa manane,  wa tarehe 12 Januari, mwaka 1964, eneo la Chukwani, ufukweni mwa Bahari ya Hindi, kisiwani huko, alionekana msichana mmoja mrefu, mwembamba wa kadri, mwenye umri wa miaka ishirini hivi. Msichana yule wa Kiarabu, aliyekuwa ameumbika ipasavyo, alionekana kama kivuli usiku ule, na pia alikuwa amejifunga upande mmoja wa khanga, huku akiwa ameongozana na kijana mmoja wa kiume, mwenye umri mkubwa kuliko yeye.
Wote wawili walikuwa wakitweta kutokana na mbio walizokuwa wanakimbia kuokoa maisha yao yaliyokuwa hatarini. Kwenye mkono wake wa kulia, msichana huyo alikuwa ameshika kijimkoba kidogo cha ngozi, alichokuwa amehifadhi vitu viwili tu, baibui lake jeusi, na kitabu kidogo cha Kiarabu, ambavyo vilitosha kwa safari yake iliyokuwa na mashaka mazito. Hawakujua mwisho wao utakuwaje!
Muda wote waliokuwa wakikimbia, mara nyingi walikuwa wakijibanza katika kuta za majumba hadi walipofika ufukweni mwa bahari. Na hata baada ya kufika huko, hawakuridhika na hali ile waliyokuta huko, kwani iliwabidi pia kujificha katika vichaka vilivyokuwa vimezunguka eneo hilo. Hawakuamini kama katika kukimbia kwao, wasingekutana na wale wananchi waliokuwa na hasira kali, ambao walikuwa wakiua watu ovyo, hususan wenye asili ya Kiarabu!
Msichana huyo alijulikana kwa jina la Salma binti Mahmoud Karama, ambapo mbele yake, alikuwa amemtangulia yule kijana wa kadri, ‘Mswahili’, ambaye mwili wake ulionyesha kudhoofika kutokana na kufanya kazi za suluba, zisizo za mapumziko, alizokuwa anafanya akiwa ni kitwana katika familia za Kiarabu. 
Kijana huyo alijulikana kwa jina la Awadh Ngwashani, na alikuwa na umri wa miaka ishirini na minne hivi. Yeye alikuwa ni mfanyakazi wa nyumbani katika nyumba ya ukoo wa kimwinyi, ambapo msichana yule alikuwa ametokea usiku ule wa mashaka, usiku wenye hofu! Ni usiku ule wa mapinduzi dhidi ya utawala wa kimwinyi, kule Visiwani, na mambo yakawa magumu kwenye mitaa mingi iliyosongana, kama vile, Darajani, Mlandege, Shangani, Malindi na Baraste, nyuma ya Marikiti kuu, Unguja, kuelekea usawa wa Ngome Kongwe.
Ni sehemu iliyokuwa nyumbani kwa wazazi wa Salma, Mzee Mahmoud Karama na mkewe, Bi. Zuleka Barafaa, ambao waliuawa kwa kuchinjwa kama kuku! Waliuawa na wananchi waliokuwa na hasira kali, ambao walikuwa wakipambana dhidi ya Utawala wa Kisultani, katika kuwaondoa madarakani. Basi, kati ya waliofanikiwa kuokoka katika familia ile, alikuwa ni msichana, Salma ambaye alipenya katika uchochoro uliokuwa unatokeza upande wa pili wa nyumba yao, na hatimaye akamchukua yule mtumishi wao, Awadh, halafu wakakimbilia ufukweni mwa Bahari ya Hindi, eneo la Chukwani, mbali kabisa na mji wa Unguja, ili kutafuta namna ya kujiokoa. Ni sehemu ambayo walikuwa wanahifadhi vyombo vyao vya uvuvi, ambapo kijana yule alikuwa anapafahamu vizuri.
Hatimaye baada ya kujificha kwa muda na kuhakikisha kuwa hali ilikuwa ni ya usalama, walijitokeza ufukweni mwa bahari na kupumzika kwa muda ili kupata nguvu mpya na kujua cha kufanya. Na hapo Chukwani, ufukweni mwa bahari, palikuwa na baadhi ya majahazi  yamepaki, na katikati palikuwa na boti moja kubwa, ambayo ilikuwa inatumiwa na familia ile ya kimwinyi.
Baada ya kuikagua vizuri, Awadh alikuta ina mafuta ya kutosha, ukizingatia ilikuwa ni kawaida yao baada ya kuitumia, huwa wanajaza mafuta kabisa, na mengine huyaweka ya akiba. Kwa haraka, wote wawili walipanda ndani ya boti hiyo, na Salma akamwamuru Awadh aiondoe  kuielekeza upande wa Tanganyika, ili kuikwepa misukosuko ile ya Mapinduzi ya Unguja.
Awadh Ngwashani hakupenda kuipinga amri ile ya mtoto wa kimwinyi, haraka akaitia moto injini, na kuiondoa boti, kuelekea katikati ya bahari, huku nyuma wakiendelea kusikia vilio na mayowe ya kuomba msaada, kwa baadhi ya familia za kiarabu zilizokuwa zikangamizwa katika mapambano hayo. 
Ni matata mazito!
Usiku ule giza lilikuwa zito kiasi cha kuongeza hali ya wasiwasi, na boti iliendelea kukata mawimbi. Bahari nayo ilikuwa shwari wala hakukuwa na mawimbi yoyote ambayo yameizuia safari yao ile ya kuzikimbiza roho zao. Kijana Awadh alikuwa akiiongoza vizuri na mngurumo wa injini iliyokuwa ikifanya kazi ulisikika na kuukimbiza ukimya ule!
Kwa muda wote ule, msichana, Salma alikuwa amejikunyata pembeni mwa boti, huku akitetemeka kwa baridi kali iliyokuwa inavuma baharini, kwani hakuwa na nguo nzito ya kujisetiri zaidi ya ule upande wa khanga. Salma alikuwa akimwangalia jinsi Awadhi alivyokuwa analiongoza boti ile kwa umakini mkubwa. Hata hivyo, Awadhi ambaye wakati wote alikuwa akimhurumia, akamwambia kwa sauti ya chini:
“Salma…”
“Bee…” Salma akaitikia kwa sauti ya chini huku akimwangalia Awadh, ambaye kwa muda ule alimwona kama mwokozi wake mkubwa. Hakumwona kama alikuwa ni mtwana wao, aliyekuwa kwa kiasi fulani akimdharau!
“Hali ni mbaya sana huko tulikotoka…” Awadh akamwambia kwa sauti iliyojaa mashaka pia.
“Ni kweli…” Salma akasema na kuongeza. “Hali ni mbaya sana…ni mapinduzi…wananchi wa Unguja wameamua kuuangusha utawala wa Kisultani…oh, ni mauaji…wazazi wangu wote wameuawa!”
“Hakuna jinsi…maadam umeiokoa roho yako, shukuru Mungu…”
“Nimeokoka lakini nina uchungu sana, sijui wazazi wangu wamewakosea nini masikini!”
“Ni sawa una uchungu. Lakini tujiulize tunaelekea wapi?” Awadh akauliza huku akimwangalia Salma. Kwa kiasi fulani yeye alifurahi kwa kuondolewa kwa utawala ule wa Kisultani uliokuwa wa manyanyaso makubwa dhidi ya watu wengine!
“Tunakwenda Tanganyika Bara…” Salma alimwambia Awadh.
“Unasema tunakwenda Tanganyika?” Awadh akamuuliza kana kwamba alikuwa hajamwelewa!     
“Ndiyo, tunakwenda huko...” Salma akamwambia kwa msisitizo.
“Tutafikia wapi masikini?”
“Tutakapofikia tutajua hukohuko, ili mradi roho yangu imepona…”
“Sawa dada’ngu…” Awadh akasema kwa sauti ndogo, huku akiendelea kuiongoza boti ile iliyokuwa ikikata mawimbi kwa kasi.
Ingawa pia Awadh angeweza kumdhuru Salma kwa kile alichokiita kulipa kisasi kutokana na kutawaliwa kwa muda mrefu, lakini hakutaka kufanya hivyo zaidi ya kumsaidia mpaka mwisho wake. Ukweli ni kwamba alikuwa akifanya kazi kwa manyanyaso makubwa na bila kuthaminiwa utu wao, katika familia zile za kimwinyi. Mswahili yeyote alionekana si kitu mbele yao, wewe ni wa kutumikishwa tu!
Boti iliendelea kukata mawimbi kuelekea upande wa Tanganyika. Kwa vile Awadh  alikuwa mtaalamu wa chombo kile, hakikumpa shida. Aliweza kukiongoza vizuri, huku baharini wakikutana na wavuvi waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za uvuvi, wengine wakiwa hawajui kilichotokea kule Unguja, kama kulikuwa na mapinduzi ya umwagaji damu!
Wakati ambao wao walikuwa baharini, pia, walikuwepo askari polisi wa Utawala wa Sultani, na wananchi wengine, kama waliokuwa wanayakimbia machafuko yale, kuelekea upande wa nchi ya Tanganyika na kwingineko, ili mradi waokoe roho zao!
Hakuna aliyemsemesha mwenzake kwa wakati ule!
Ni kuokoa uhai, na si vinginevyo!

          ********
Wakati boti ile ikiendelea na safari, mwanadada, Salma alikuwa bado amejikunyata na mawazo yake yakiwa mbali sana juu ya tukio zima lilivyotokea usiku ule. Mawazo yale yalikuwa yakitiririka kama vile ilikuwa ni sinema. Alikumbuka kuwa saa mbili za usiku ule, wakiwa familia nzima ya kimwinyi, ndani ya nyumba yao ya kifahari, iliyoko juu ghorofani, eneo la Baraste, mjini Unguja, walikuwa wakila chakula cha pamoja, ukiwa ndiyo utaratibu wao waliokuwa wamejiwekea.
Alikuwepo baba yake, Mzee, Mahmoud Karama na mama yake, Bi. Zuleka Barafaa. Wengine ni kaka zake wawili, Ramadhani na Farouk, ambapo kwa watoto, walikuwa watatu tu, wawili wa kiume, na yeye wa kike wa pekee.  Basi, usiku ule walikula chakula huku wakiongea hili na lile, hasa kwa wazazi wake walivyokuwa wakiongea kwa furaha, huku wakipanga mipango yao ya baada ya kuongeza miradi yao ya mashamba ya minazi na karafuu, na pia kuajiri wafanyakazi wa kiume, zaidi ya Awadh, kwa ajili ya shughuli zile za shamba na za uvuvi  kwa ujumla.
Baada ya kuongea mambo mengi na kutosheka, ndipo walipoagana na kuahidiana kukutana kesho yake, kwani usiku ni mwaka. Wakaingia vyumbani mwao na kulala, ikiwa imetimu saa nne za usiku. Salma  alikumbuka kuwa, aliagana na wazazi wake kama ilivyokuwa wamezoea, kisha akaingia ndani ya chumba chake na kulala, kilichokuwa kinatazamana na mtaa mdogo uliokatiza kwa upande wa chini kutoka ghorofani.
Kaka zake, Ramadhani na Farouk, nao waliingia ndani ya vyumba vyao na kulala. Nyumba yao ilikuwa katika ghorofa ya pili, katika majumba yale ya kizamani ya Mji Mkongwe, eneo la Baraste, ambayo nayo baba yao aliirithi kutoka kwa baba yake, miaka mingi iliyopita.
Kwa jumla, Salma alipokwenda kulala, hakujua kitu ambacho kingetokea kwa usiku ule, kwani wakati wao wakiwa wamelala usingizi mzito, huku nyuma, wananchi waliokuwa wamechoshwa na utawala wa kisultani, wenye manyanyaso, walikuwa wamepanga kufanya mapinduzi makubwa, kuung’oa utawala wake.
Hivyo basi, katikati ya usiku wa manane, ndipo Salma akiwa katika usingizi mzito, ndipo aliposikia makelele ya watu waliokuwa wakilia na kupiga mayowe ovyo!  Haraka, Salma akatupa shuka lake na kuamka! Akanyanyuka kutoka kitandani, kisha akaenda kuchungulia dirishani kutoka juu. Baada ya kuchungulia nje, ndipo kwa chini, Salma aliweza kuona wananchi wengi, wakiwa wamebeba silaha za aina mbalimbali kama bunduki, mapanga, mikuki na nyinginezo.
Watu wale walikuwa wakivamia nyumba moja baada ya nyingine zilizokuwa zinakaliwa na mamwinyi wa Kiarabu. Baada ya kuzivamia, wakawa wanawatoa nje na kuwapiga hadi kufa, na wengine wakiwachinja hadharani kama kuku, bila kuwa na huruma yoyote!
Hatimaye na nyumba yao ikavamiwa na watu wale wenye hasira, kuanzia ghorofa ya chini ilipokuwa inaishi familia nyingine ya kimwinyi, ambayo ilitolewa nje mmoja baada ya mwingine, na kuuawa kwa kuchomwa mikuki hata kuchinjwa na majambia!  Salma alikuwa akishuhudia!
Hivyo alichofanya haraka Salma, ni kuvalia upande wa khanga, na nguo ya ndani tu, hakuwa na muda wa kuvalia nguo, hasa ukizingatia milango yao ndiyo kwanza ilikuwa inavunjwa na wananchi wale wenye hasira kali!
Baada ya kuvalia ule upande wa khanga, Salma alikimbilia ndani ya kabati na kuchukua mkoba wake mdogo wa ngozi, ambapo pia, alichukua baibui lake, na kitabu kidogo cha Kiarabu, ambacho kwa upande wake kilikuwa na umuhimu wa pekee kwa siku ile ya aina yake.
Alipofanikiwa kuchukua vitu vile vya pekee, akachomoka ndani ya chumba chake na kutokea verandani. Alipofika pale verandani, akakuta watu wale wameshaingia ndani na muda ule walikuwa wakiwashambulia wazazi wake, baba na mama yake, ambapo alishuhudia wakichinjwa kama kuku na kuachwa wakitapatapa na kukata roho.
Pia, alishuhudia kaka zake, Ramamadhani na Farouk wakichinjwa hadi kufa, huku wakiachwa katika ngazi za kupandia.  Wauaji wale wakawa wanamtafuta yeye, lakini hawakumwona, kwani muda ule, Salma alikuwa amejichimbia chini ya meza moja kubwa, iliyoweza kumficha kutokana na giza lililokuwepo mle ndani baada na umeme kukatwa mji mzima. Wauaji hawakumwona!
Kwa vile walikuwa na haraka sana, baada ya kuhakikisha wamemaliza kufanya mauaji yale, watu wale waliondoka na kuelekea katika nyumba nyingine kuendelea na mauaji yale dhidi ya mamwinywi! Ukweli ni kwamba walikuwa wamejipanga ipasavyo kwa kile walichokuwa wamekifanya.
Salma alipohakikisha watu wale wameondoka, ndipo alipotoka na kuteremka chini kwa kutumia ngazi ya nyuma inayotokea sehemu ya uani. Baada ya kufika huko, ndipo alipomkuta kijana, Awadh, mtumishi wao, akiwa naye anajichomoa kutoka katika uchochoro mmoja wenye giza, aliokuwa amejificha huko punde tu wauaji wale walipofika na kuivamia nyumba ile.
Mtumishi Awadh, yeye alikuwa anaishi katika chumba kimoja, ambacho pia hutumika kama stoo ya kutunzia vitu, iliyokuwa kule chini mwanzo wa ghorofa. Ndiyo maana akashtuka mapema!
“Salma!” Awadhi alimwita kwa sauti ndogo!
“Beee!” Salma akaitikia huku akimwangalia Awadhi. Hakutegemea kumwona kwa wakati ule!
“Umesalimika?” Awadhi akamuuliza!
“Ndiyo, nimesalimika, lakini baba, mama na kaka zangu, wote wameuawa!”
“Hata mimi nimenusurika, cha muhimu tuondoke eneo hili haraka sana!”
“Sawa, tuondoke,” Salma akasema na kuongeza. “Lakini tunakwenda wapi?”
“Wewe twende tu, tutajua huko mbele ya safari!”
Awadh na Salma wakatoka ndani ya nyumba ile kwa kutumia mlango wa uani. Huku Awadh amemshika mkono Salma, wakaanza kukimbia huku wakiufuata mtaa mmoja mwembamba katika ule mji mkongwe, ambapo pia walikutana na watu wengine waliokuwa wanakimbia ili kuyanusuru maisha yao. Pia, waliweza kukutana na maiti nyingi za watu zikiwa zimelala barabarani, na madimbwi makubwa ya damu yakiwa yametapakaa!
Hata hivyo, Awadh na Salma waliendelea kukimbia hadi walipotokea eneo la Chukwani, ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Huko nyuma makelele ya watu yalikuwa yakiendelea kusikia, pamoja na milio ya bunduki za rashasha zikilipuka mara kwa mara.
Ni kizaazaa!        
“Tunakwenda wapi Awadh?” Salma aliendelea kumuuliza.
“Tunaokoa roho zetu Salma!” Awadh akamwambia huku wakiendelea kukimbilia uelekeo wa baharini.
“Hivi huku si kuna ile boti ya uvuvi?” Salma akamuuliza Awadhi.
“Ndiyo, iko huku...na ndiyo huko tunaelekea!”
“Hakuna jinsi, tutoroke nayo...”
“Umesema jambo la maana Salma!” Awadh akamwambia huku wakiendelea kukimbia kwa tahadhari ya hali ya juu, na pengine wakijikinga kwenye vichaka kama kutakuwa na adui asiwaone!
Hatimaye mbio zao ziliishia pale ufukweni mwa bahari. Wakaifikia ile boti kubwa inayotumia injini, yenye uwezo wa kubeba watu kumi kwa mara moja. Baada ya kuikagua haraka haraka, Awadh alikuta ina mafuta ya kutosha, pamoja na ya akiba, kwa safari yao ile yenye mashaka mazito!
Mayowe ya watu yaliendelea kusikika mara dufu, kiasi cha kuendelea kuwapa wasiwasi mkubwa!
Ndipo Awadh alipoitia moto boti ile, halafu akaiondoa  kwa mwendo wa kasi kuelekea wasipopajua, na mwishowe wakaamua kuelekea nchini Tanganyika!
Hivyo ndivyo ilivyokuwa!

          *******
Baada ya saa nne hivi za hekaheka ndani ya bahari, hatimaye, kijana Awadh na mwanadada, Salma, walifanikiwa kufika ufukweni mwa Bahari ya Hindi, upande wa Tangayika, wakati huo kukiwa kumeshapambazuka. Awadh akatia nanga na wote wakashuka chini huku wakikanyaga maji ya bahari na kwenda kukaa katika mchanga, kando ya bahari, wakabaki wanatafakari. Njaa kali na kiu ya maji ilichukua sehemu yake katika matumbo yao, lakini hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awasaidie, na walikaa pale ufukweni, wamejilaza mchangani, kwa muda wa saa nzima.
Hawakuamini kama walikuwa wamesalimika katika mapinduzi yale yaliyotokea usiku ule wa manane, hivyo wakaendelea kukaa na pia wakiangaza macho yao huku na kule, na kuangalia mandhari ya eneo lile walilofikia. Palikuwa kimya kabisa, kukiwa kumezungukwa na miti ya minazi iliyofungamana, ingawa pia, paliweza kuonekana baadhi ya vyombo, kama mitumbwi na majahazi yaliyokuwa yameegeshwa pale ufukweni.
Awadhi na Salma wakapata matumaini ya kusaidiwa na wavuvi watakaokuwa wanarudi kutoka katika shughuli za uvuvi. Hivyo wakakaa chini kwenye mchanga huku wakiwa taabani kwa uchovu. Baada ya kukaa kwa muda, ndipo walipomwona mtu mmoja, kijana, ambaye kimtazamo alionekana kuwazidi umri kiasi, pia alionekana kama ni mvuvi kutokana mavazi yake aliyovalia. Alipowaona wamekaa pale ufukweni, chini ya mchanga, aliwaendea kwa mwendo wa taratibu, huku pia akiiangalia boti yao pale ilipokuwa imetia nanga.
Ukweli ni kwamba mvuvi yule alikuwa akiwashanga baada ya kuwaona wakiwa katika sehemu ile, kwa muda ule, tena wakiwa na boti ile, ambayo kwa wakati ule ilionekana ya fahari sana, kwani ni watu wachache sana waliokuwa wakimiliki chombo kama kile, hususan, Wazungu, Wahindi, Waarabu na wengineo wenye uwezo wa kifedha. Na pia, vijana hao hawakuonyesha dalili zozote kama walikuwa ni wavuvi!
“Habari zenu…” kijana yule mvuvi, ambaye hakupishana sana kiumri na Awadhi aliwasalimia huku akiwaangalia kwa makini kuanzia juu mpaka chini.
“Hatujambo…” Salma akaitikia huku naye akimwangalia kwa wasiwasi. Mwili wake ulikuwa bado unatetemeka kwa baridi na hofu kubwa iliyokuwa bado imemtawala.
“Vipi jamani…mbona mko hapa saa hizi?” Mvuvi yule aliendelea kuwauliza, na pengine akiwakagua. Hawakuonyesha kama ni watu waliokuwa wanajishughulisha na shughuli za uvuvi, kwani hawakuwa na zana zozote za uvuvi.
“Sisi tumepotea baharini…” Salma akamwambia kwa kumdanganya.
“Mmepotea baharini?” Kijana huyo akauliza.
“Ndiyo, tumepotea, na hatuna sehemu ya kufikia…” Salma alimwambia mvuvi yule kwa kumdanganya.
Salma hakupenda kumweleza ukweli kwamba walikuwa wamekimbia Kisiwani Unguja, baada ya Mapinduzi yaliyokuwa na mauaji ya kutisha yaliyowaacha watu wengi wamekufa!
“Mmetokea wapi?” Mvuvi yule akauliza tena.    
“Tumetokea Visiwa vya Ngazija…” Salma akaendelea kudanganya.
“Visiwa vya Ngazija?”
“Ndiyo...” akaendelea kusema Salma bila kumwachia Awadh aongee.
“Ooh, mbali sana!”
“Tumechoka kweli…tunaomba msaada wako...” Awadh naye akajitutumua.
“Na pia njaa na kiu ya maji inatuuma sana…” Salma akaendelea kusema akitegemea kupata fadhila kutoka kwa yule mtu.
“Oh, poleni sana…nitawasaidia…” mvuvi yule akawaambia na kuonyesha ni mtu muungwana.
“Tunashukuru sana,” Salma akasema kwa sauti ya upole.
“Sasa, hii boti yenu ni ya thamani kubwa.”
“Ni kweli, ina thamani kubwa, sasa tuiache hapa hapa?”
“Hiyo boti iacheni hapahapa, kwani ni sehemu ya usalama na nitaikabidhi kwa walinzi. Ngoja nitaongea nao, watailinda pasipo tatizo lolote...” mvuvi yule akawaambia, nao wakamwelewa. Kwa kiasi fulani matumaini yakawajia.
 “Sasa kabla ya mambo mengine, inawapasa kwanza mpate kifungua kinywa, kwani mmekaa sana baharini. Na pia mmepigwa na baridi kali, hebu nifuateni…” mvuvi yule akaendelea kuwaambia.
“Sawa,” Salma akasema huku akimwangalia kwa makini.
Kisha yeye na Awadhi, wakamfuata nyuma yule mvuvi kwa hatua za kichovu. Wakalitoka eneo la ufukweni na kutokeza upande wa juu, katika mitaa kadhaa ya jiji, huku wakiyatupa macho yao pande zote ukizingatia wote wawili walikuwa ni wageni kabisa na ni mara yao ya kwanza kufika, upande wa pili, Tanganyika katika enzi hizo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Pia, ndiyo kwanza Tanganyika ilikuwa imetimiza miaka minne tu tokea ijinyakulie Uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Tuseme walikuwa hawajafika hasa katika jiji la Dar es Salaam, ambalo ni karibu na kisiwa cha Unguja.
Lakini kabla mvuvi yule muungwana hajawapeleka nyumbani kwake, walipitia katika hoteli moja iliyokuwa katikati ya jiji. Wakaingia ndani ya hoteli hiyo, ambapo mtu yule aliwaagizia chakula cha kutosha, ambapo waliendelea kula taratibu hadi waliposhiba. Wakati wakiendelea kula, mwenyeji wao alikuwa akiwasubiri mpaka walipomaliza kula na kumshukuru kwa wema aliowafanyia
Hakika Salma akajisikia ahueni, kwani njaa aliyokuwa nayo ilikuwa karibu imtoe roho, ukizingatia yeye alikuwa ametokea katika familia ya ki-mwinyi ambayo haikujua shida ni kitu gani, basi akawa anatafakari ya mbele yake. Akakubaliana na hali ile iliyotokea nyumbani kwao Unguja, kwamba ukoo wake mzima umeteketea!

          *******
Ndani ya kisiwa cha Unguja, kulipambazuka kukiwa bado na pilikapilika za watu waliokuwa wakishangilia juu ya mapinduzi yale yaliyomwondoa Sultani madarakani. Kiongozi wa mapinduzi yale, Field Marshal John Okelo, alikuwa akizungushwa mji mzima, akiwa kwenye gari la wazi, aina ya Land Rover, pamoja na wapambe wake waliowezesha kufanyika kwa mapinduzi yale.
Watu wengi walikuwa wamejaa katika mitaa na maeneo mengi ya mji wa Unguja, wakimshangilia, huku wengi wao wakiwa wamejifunga matawi ya makuti ya minazi, kichwani na viunoni. Mitaa mingi, kama vile Darajani, Mlandege, Kwahani, Jang’ombe, Saateni, Makaburi kikombe, Kibandamaiti, Kariakoo, Mwembe Mimba. Mnazi Mmoja, Mwanakwerekwa na kwingineko, kulikuwa kumejaa shamrashamra nyingi. Vilevile mbali ya hao, waliweza kuonekana askari wa mapinduzi yale wakiwa doria mitaani kwa kuwahimiza wananchi wabaki na amani, wasiwe na wasi wasi wowote.
Kambi kuu ya Askari Polisi, ya Ziwani, almaarufu kwa jina la ‘Ngomeni,’ ilikuwa imetekwa, ikiwa chini ya askari wa kimapinduzi, na baadhi ya askari waliokuwa chini ya utawala wa Kisultani, walikuwa wameuawa, na wengine walijisalimisha na kubaki upande wa wanamapinduzi.
Hakika kulikuwa na pilikapilika nyingi, huku pia magari maalumu yalikuwa yakipita nyumba kwa nyumba, hasa zile za ma-mwinyi, na kuziondoa maiti za wale watu waliouawa usiku wa jana yake, na kuzipelekea katika Hospitali ya  V. I. Lennin, siku hizi, Hospitali ya Mnazi Mmoja, ili kuzihifadhi, na kusubiri taratibu za mazishi ya pamoja.
Damu ilikuwa imetapakaa kila kona na kuonyesha ni jinsi gani watu wale walivyouawa kinyama! Upande wa pili, kwenye nyumba moja ya ghorofa mbili, iliyoko eneo la Baraste, Mji Mkongwe, nyumba aliyokuwa anaishi Salma, palikuwa pamepoa kimya, punde askari wale walipokuwa wanapita kuzichukua maiti zile. Ghorofa ya kwanza, watu wote wapatao sita, walikuwa wameuawa, na maiti zao zilikuwa zimetapakaa kwenye uwanja mdogo wa nyumba hiyo.
Baada ya maiti zile kuchukuliwa na kupakizwa ndani ya lori kubwa aina ya Bedford, askari wale walipanda hadi juu, katika ghorofa ya pili, waliyokuwa wanaishi familia ya akina Salma. Kwenye ngazi za kupandisha juu, walizikuta maiti mbili, zikiwa ni za mzee Karama, na Bi, Zuleka, wazazi wa Salma. Na pia baada ya kufika juu, kwenye varanda, kulikuwa na maiti mbili, za Ramadhani na Farouk, kaka zake Salma. Maiti zile zikachukuliwa na kupelekwa kuhifadhiwa hospitali, na pale ndipo ilimaanisha kuwa ukoo mzima wa akina Salma ulikuwa umeteketea wote!
Maeneo ya mashambani, nje ya mji, kama Mahonda, Bububu, Mwera, Machui na kwingineko, mamwinyi walisambatatishwa na hata wengine kuchomewa ndani ya nyumba zao. Mashamba ya minazi na mikarafuu ikatwaliwa na wazawa. Hakika hali ilikuwa bado ni ya kutisha, kwani vilio vya uchungu vilikuwa vimetawala kila kona, kwa familia zile zilozoathirika!
Na kilichofanyika pale, ni milango yote ya nyumba ilifungwa kwa makomeo, ili watu wale wasiweze kurudi tena katika makazi yale, ukizingatia wao walikuwa ni mamwinyi waliokuwa wanaunga utawala wa kisultani. Kwa hivyo makazi yale yalitegemewa kuja kuingia wazawa wa kawaida, ambao walikuwa na uchungu na utawala ule uliokuwa wa unyanyasaji mkubwa!

*******  
Jijini Dar es Salaam.
kijana yule msamaria mwema, aliyewafadhili Salma na Awadhi, alijulikana kwa jina la Karim Kizango. Hakupoteza muda, baada ya kuhakikisha  wageni wale wameshiba, aliwachukua hadi kwenye kituo cha mabasi, ambapo walipanda basi hadi Kariakoo. Baada ya kufika, walishuka, halafu akawapeleka  mpaka nyumbani kwake, katika mtaa wa Livingstone, eneo hilo la Kariakoo, ambapo alikuwa na nyumba yake.
Ilikuwa ni nyumba yenye ukubwa wa wastani, iliyojengwa kwa udongo na kurepewa kwa saruji, kama  zilivyojengwa nyumba nyingine katika mtaa ule maarufu katika enzi zile za mwanzo wa uhuru wa Tanganyika. Kwa ujumla, nyumba ile pia, ilikuwa imeezekwa kwa mabati, ambayo yalikuwa yameshaanza kubadilika rangi, na kuwa ya kutu kutokana na mvuke wa maji ya chumvi.
Ni nyumba ambazo kwa kiasi fulani zilikuwa katika kiwango cha chini, ukizingatia kipindi kile ndiyo kwanza nchi ya ilikuwa imepata Uhuru  kutoka kwa mkoloni wa Kiingereza, katika miaka ile ya sitini. Wananchi wengi hali zao zilikuwa duni kwa sababu ya kutawaliwa na kutengwa kimatabaka.
Ina maana kuwa watu walikuwa wakiishi kimatabaka, mfano, Wazungu, Wahindi na Waswahili, hawakukaa pamoja, kila mmoja kivyake! Ingekuwa siyo rahisi kwa Mswahili kwenda kujenga nyumba eneo analoishi Mhindi, au Mzungu. Utachukuliwa hatua kali!
Mzungu aliishi uzunguni!
Mhindi aliishi  Uhindini katikati ya jiji!
Mswahili aliishi Uswahilini, nje ya jiji, kama vile, Buguruni, Manzese, Magomeni, Ilala na kwingineko!
Kwa mtu kama Karim Kizango, kwa enzi zile alionekana ni mtu wa kati, kwa kufanikiwa kuwa na nyumba mjini, licha ya kufanya ile kazi ngumu ya uvuvi, iliyowafanya watu wamwite kwa jina la Karim  ‘Mvuvi’, badala ya jina lake halisi. Nyumba ile iliyokuwa inatazamana na mtaa ule, ilikuwa ni ya nne tu kutoka katika makutano ya mtaa ule na mtaa wa Kichwele, ambao baadaye ulikuja kuitwa mtaa wa Uhuru. Ni nyumba iliyokuwa na vyumba sita, ambapo vyumba vitatu vilikuwa vimepangishwa na viwili akivimiliki Karim mwenyewe. Pia, upande wa uani palikuwa na chumba kingine, ambapo kiliambatana na banda la stoo na choo.
Baada ya kuwafikisha Salma na Awadh, aliwakaribisha, ambapo walifikia katika chumba kile, ambacho alikitenga maalum kwa wageni. Wakaingia na kujikalia kwenye samani ambazo hazikuwa za gharama, ni viti vya kawaida kama vile vinavyotumika ofisini. Salma, akiwa bado amechanganyikiwa, baada ya kuingia mle ndani, akawa akikikagua kile chumba kuanzia pande zote, na pia, Awadhi naye alikuwa akiyazungusha macho yake pande zote za kuta nne.
Kilikuwa ni chumba kikubwa kama vilivyokuwa katika nyumba nyingi enzi zile. Upande wa kulia palikuwa na kabati la mbao lililokuwa na vyombo vya udongo, vya chakula vilivyopangwa vizuri, sahani na vikombe vya chai.  Pia, kulikuwa na vifaa vya kuhifadhia maji ya kunywa, ndoo mbili tatu, meza ya kulia chakula iliyokuwa na viti kama vile walivyokuwa wamekalia.
Ukutani palikuwa na saa iliyotundikwa, ambayo ilikuwa na kengele inayocheza kushoto na kulia, iliyoundwa kwa mbao. Chini sakafuni, palikuwa na zulia zuri lililotandikwa na kuenea chumba kizima. Vyote hivyo, viliweza kumtambulisha Karim alikuwa ni mtu wa aina gani. Ni mtu mwenye uwezo wa wastani kimaisha.
“Karibuni jamani, hapa ndiyo nyumbani kwangu,” Karim aliyekuwa amekaa kwenye kiti kingine akawaambia Awadh na Salma.
“Ahsante, tunashukuru sana,” Salma akasema.
“Tunashukuru sana...” Awadh naye akaongeza.
“Tafadhali, mjisikie kama mko nyumbani, pumzikeni  kwanza. Baadaye ndiyo tutaweza kuongelea kilichowasibu, na juu ya kuweza kuwasaidia kwa kile mnachohitaji kusaidiwa.”
“Tunashukuru sana...”
Salma na Awadh walipumzika kwa siku ile, huku Karim akifanya mipango yote ya kuwatafutia nguo nyingine za kubadilisha, ukizingatia kule walipokuwa wametokea, hawakufanikiwa kuchukuwa nguo za kubadili, kwani walikuwa wakikimbia kuokoa maisha yao.  Basi, Salma aliweza kununuliwa magauni, khanga na nguo nyinginezo zinazomhusu mwanamke, na Awadh kadhalika, alinunuliwa mashati na suruali, wakaonekana tena watu katika watu.
Wakati wote ule habari za mapinduzi ya Unguja yalikuwa yametapakaa kote nchi nzina na nje ya nchi. Hakika hata nchini Tanganyika, yalijenga hofu kuu na taharuki, hasa kwa vile kisiwa cha Unguja kiko jirani na tu, na ni watu waliokuwa wanatembeleana mara kwa mara. Vyombo vya habari vilikuwa vinatangaza tukio lile kwa mapana na marefu, kiasi cha kuwafanya watu wakae katika makundi mitaani, wakizungumzia jambo lile lililotokea bila kutegemea kwa kuunganisha nguvu ya umma! Watu waliochoka kutawaliwa na kunyanyaswa katika ardhi yao!
Watu wengi sana walikuwa wamekufa usiku ule wa mapinduzi, wakiwemo wazazi na kaka zake, Salma. Viongozi walioshiriki katika mapinduzi yale wakajitangaza na kuchukuwa uongozi wa visiwa vile, huku Sultani akiwa ametorokea nchini Uingereza kwa usafiri ambao mpaka muda ule hakuna aliyejua jinsi alivyofanikiwa kuchoropoka mikononi mwa watu waliokuwa na uchungu wa kumtoa roho yake!
Habari zile za mapinduzi ya Unguja, Karim Kizango alizipata kwa mapana na marefu siku ile ile alipowapokea watu wale, Salma na Awadhi. Machale yakamcheza, akahisi kuwa wageni wale walikuwa ni moja ya watu waliokuwa wameyakimbia mapinduzi yale na kumdanganya kuwa walikiuwa wamepotea baharini wakitokea katika Visiwa vya Ngazija.
Kilichomfanya Karim ahisi vile, ni juu ya mwanadada, Salma, ambaye alikuwa ni Mwarabu, tena aliyeonekana kutokea kwenye familia yenye unafuu wa maisha, ukiachia mbali ule usafiri wa boti nzuri na ya gharama. Lakini kwa vile alikuwa ameshawapokea, aliwasubiri kwanza wapumzike, halafu kesho yake ndipo aanze kuwapeleleza.
Kwa vile kazi za uvuvi zilikuwa zinafanyika nyakati za usiku, basi, Karim aliwaaga jioni yake na kuelekea baharini. Kabla ya kuondoka, akawaendea pale sebuleni walipokuwa wamekaa na kuanza kuongea nao.
“Jamani, nawaomba mjisikie kama mko nyumbani...” 
“Ni kweli tunajisikia tuko nyumbani...” Salma akasema.
“Hakuna tatizo bwana, tunashukuru kwa wema wako...” Awadhi naye akasema.
“Sasa, kwa vile mimi nashughulika na kazi za uvuvi, itanibidi niende...” Kizango akasema na na kuongeza. “Nitawaacha hapa nyumbani mpumzike, ambapo wewe Salma utalala chumba hiki hapo, na wewe Awadh utalala kwenye chumba hicho kingine.”
“Sawa bwana, tunashukuru sana...” Salma akasema kwa sauti ndogo lakini iliyosikika.
“Ingawa kuna hofu kubwa iliyotanda kote, itanibidi niende katika shughuli zangu, ukizingatia kuna nyavu nilizokuwa nimeshazitega baharini. Natumaini na nyie pia mmesikia habari hizo katika vyombo vya habari, juu ya mapinduzi yaliyotokea huko Unguja, usiku wa kuamkia leo!” Karim Kizango akaendelea kuwaambia.
Lakini baada ya kusema vile, Salma na Awadh wakashtuka kidogo!
“Ni kweli tumezisikia, na mpaka sasa hivi hali si shwari...Oh, Mungu wangu!” Salma akasema kwa uchungu mwingi. Machozi yakaanza kumtoka kwa wingi!
“Mbona unalia Salma?” Kizango akamwuliza!
“Ni uchungu...oh...oh!” Salma akaendelea kulia kitu ambacho kilimshangaza Karim Kizango!
“Eti, mwenzako analia nini?” Kizango akamuuliza Awadh.
“Ana matatizo makubwa sana!” Awadh akamwambia Kizango.
“Matatizo gani tena?”
“Kwanza tunakuomba radhi kwa kukudanganya kuwa tunaokea katika Visiwa vya Ngazija...”
“Kumbe mmetokea wapi?”
“Sisi tunatokea kisiwani Unguja!”
“Mnatokea Unguja?”
“Ndiyo, mimi na Salma tunatokea Unguja, kwa kuyakimbia mauaji yaliyokuwa yanaendeshwa na watu waliokuwa wameamua kuuapindua utawala wa kisultani...”
“Mh, hii mpya!” Kizango akasema huku akitikisa kichwa chake!
“Ndiyo hivyo bwana, hapa tunapozungumza, ni kwamba, wazazi wake na kaka zake wawili wote wameuawa kwa kuchinjwa kama kuku. Sisi tulifanikiwa kukimbia baada ya kujificha kiasi kwamba wauaji hawakutuona, na baada uya kufanikiwa kufika ufukweni, ndipo tulipopanda ile boti, ambayo ilikuwa inatumika kwa shughuli za uvuvi. Tukakimbilia huku, mpaka tulipokutana na wewe alfajiri ya leo...”
“Ina maana nyie ni ndugu?”
“Hapana , siyo ndugu, ni kama unavyoniona mimi ni Mswahili, na huyu Salma ni Mwarabu.”
“Ndiyo, naiona hiyo tofauti...”
“Mimi ni mfanyakazi  wao wa nyumbani, na nimefanya msaada wa haraka, kumtoroshea Salma huku, kwa vile angebakia kule, ni lazima wangemuua tu. Wauaji wanawafahamu watu wote wanaoishi katika familia za mamwinyi, akiwamo Salma, tofauti na mimi Mswahili, tena kitwana!”
“Oh, poleni sana. Sasa nimeshaujua ukweli mzima, lakini msihofu, nitawasaidia. Mtakaa hapa kwangu mpaka hali itakapotulia, mtaweza kurudi tena Unguja,” Kizango akawaambia.
“Sawa, ukweli ni kwamba tunashukuru sana.”
“Basi, mimi naondoka, mengi tutaongea kesho nitakaporudi...”
“Sawa bwana,” Awadh akasema huku akimwangalia Salma aliyekuwa anafuta machozi yake kwa upande wa khanga mpya aliyopewa na Kizango.
Baada ya kuwaaga, Karim Kizango akachukua baadhi ya vifaa muhimu vya kazi za uvuvi, halafu akaondoka huku akiufuata Mtaa wa Kichwele, hadi Mnazi Mmoja, ambapo alipanda basi la DMT (Dar es Salaam Motor Transport) enzi zile, lililokuwa linaelekea eneo la Posta ya Zamani, mpaka Kivukoni. Pale nyumbani aliwaacha vijana wale, Salma na Awadh wakiwa  wamepumzika, ambapo alipanga kuwa kesho yake atakaporudi, ndipo angejaribu kuongea nao kwa mapana na marefu, na wamwelezee kisa kizima cha kufika Dar es Salaam.
Baada ya kufika baharini, Karim Kizango, alipitia sehemu ile ilikohifadhiwa ile boti waliyofika nayo, Salma na Awadh, ambapo alikuta iko katika sehemu ya usalama kama walivyoiacha jana yake.  Nako, alikuta hofu ya mapinduzi bado imetawala kwa baadhi ya wavuvi, kiasi kwamba wengine waliamua kutokwenda katika shughuli zao za uvuvi, kuhofia kukutana na wauaji wale ndani ya bahari. Kwa upande wa Karim, hakuwa na wasiwasi ule, aliamua ajitose tu, kwani kazi ile ndiyo iliyokuwa ikimpatia kipato cha kuweka mjini. Hivyo basi, akatwa vyombo vyake na kuelekea baharini kuvua samaki, kazi aliyoizoea mika nenda rudi.
Mara baada ya Karim Kizango kuondoka kwenda katika shughuli zake za uvuvi baharini, Awadh na Salma walikuwa wamebakia peke yao pale nyumbani, Mtaa wa Livingstone. Hivyo basi, wakakaa na kuanza kuongea mambo muhimu ambayo waliona yangewasaidia katika safari yao ile ya kutafuta maisha mapya.
“Salma,” Awadh akamwita.
“Bee,” Salma akaitikia huku akimwangalia Awadh, ambaye kwa muda ule alimuona kama mwokozi wake mkuu.
“Tumeshafika Tanganyika...”
“Hilo naelewa...”
“Lakini tusijione kama ndiyo tumefika mwisho wa safari!”
“Ni kweli. Hapa tumefikia kwa huyu mtu mwema, aliyetufadhili. Hatuwezi kujua atatuhifadhi mpaka lini, ingawa yeye hajatuwekea muda...”
“Mbali ya kutuwekea muda, pia amesema mambo yakiwa shwari kule Unguja, ataturejesha. Kurudi Unguja ni jambo la muhimu sana kwa upande wangu, lakini kwa wewe, itakuwa ni vigumu sana. Watu bado wana uchungu na koo zenu, ukirudi utafikia wapi? Ni lazima watakumaliza?”
“Hilo ni kweli, sasa unanishauri kipi?”
“Cha muhimu, tukae kwanza kwa muda hapa, hali ikiwa shwari, mimi nitakwenda Unguja katika kusafisha mazingira. Mambo kama ni shwari, nitakuagiza urudi ili ukayaanze maisha upya.”
“Hilo ni jambo la maana, basi, tutafanya hivyo.”
Awadh na Salma hawakuwa na jinsi, walikubaliana na hali ile waliyoikuta, hivyo wakawa wanaishi na mwenyeji wao, Karim Kizango, kama familia moja. Walikuwa wakishirikiana kwa kila kitu bila kipingamizi chochote kwa muda wa mwezi mzima ule wa Januari waliofikia pale.
Kwa vile Karim Kizango alikuwa hajaoa, basi, Salma ndiye aliyekuwa akishughulika na kazi zote za mapishi za pale nyumbani, lakini kijana, Awadh hakutaka kukaa hivihivi bila shughuli za kufanya, kwani alikuwa akienda baharini na Karim, katika kazi za uvuvi, ambazo kwa upande wake alikuwa amezizoea. Walisaidiana na kuzidi kuongeza kipato cha kifamilia hasa ukizingatia walikuwa wanatumia kifaa kizuri cha uvuvi, boti inayotumia mashine, tofauti na mwanzo, alipokuwa anatumia mtumbwi wa kawaida tu. Kwa kiasi fulani, Karim aliridhika na wageni wake wale, na wala hakuona sababu zozote za kuwaondoa.


*********
Baada ya miezi mitatu kukatika, Salma na Awadh walishakuwa wenyeji ndani ya jiji la Dar es Salaam, nchini Tanganyika. Basi, huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha ya kinyumba, kati ya Karim Kizango na Salma binti Mahmoud Karama, msichana wa Kiarabu aliyemfadhili. Baada ya kukaa kwa muda mrefu na kuzoea, wakajikuta wakishirikiana kimapenzi, ukizingatia Karim hakuwa na mke, hivyo akaona ni vyema amwoe Salma awe mke wake. Salma alikubali hasa ukizingatia asingeweza tena kurudi kisiwani Unguja kwa hofu ya kuuawa, na pia familia yake yote ilikuwa imeteketezwa!
Lakini  kwa kijana Awadh, yeye aliamua kurudi Kisiwani Unguja, kwa  kuendelea na kazi za uvuvi alizokuwa amezizoea. Hakupenda kuendelea kuishi Dar es Salaam tena akiwa amefadhiliwa na Karim Kizango. Vilevile kile kitendo cha Karim kuishi kinyumba na Salma hakikumfurahisha kabisa, aliona kama Salma alikuwa amelazimishwa kutokana na hali ile ya uyatima iliyomkuta baada ya wazazi wake kuuawa.
Mnamo tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 1964, nchi za Tanganyika na Unguja viliungana na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nchi zile ziliungana chini ya Waasisi wa Mataifa hayo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume. Hivyo hali ilikuja kwa shwari na wananchi wakawa wanaishi vizuri, huku makovu yale ya kimatabaka yakawa yanafutika. Basi, pale ndipo kijana, Awadh alipoamua kufungasha virago vyake na kurudi Unguja kuendelea na shughuli nyingine, akamwacha Salma akiishi na Karim, kama mke na mume.
Katika Mtaa ule wa Livingstone, miaka ile ya sitini, wakazi wengi walimwonea wivu Karim kwa kujipatia mke mrembo  wa Kiarabu, ambaye hawakujua amempata wapi. Hata hivyo Karim na Salma walipendana bila kuwajali majirani walikuwa wanasema nini. Pia, taratibu akaanza kuisahau hali ile iliyowakuta wazazi wake waliouawa katika mapinduzi yale ya Unguja. Vilevile hakuwa na muda wa kwenda huko tena, kwani familia nzima ilikuwa imeangamizwa na nyumba yao kutaifishwa, hivyo hakuwa na sehemu ya kufikia tena, zaidi ya kumuona Karim ndiye baba na mama yake!
Na hata Salma alipoonyesha hali ya ujauzito, Karim alifurahi sana na kuzidi kumpenda Salma na kumuona kama mboni ya jicho lake! Akamtimizia kila alichokuwa anahitaji ili asisononeke. Na yote ile ilikuwa ni kwa sababu Karim alikuwa bado hajazaa mtoto, na yule alihesabu kuwa angekuwa ndiye mtoto wake wa kwanza katika maisha yake, hivyo basi hakuwa na budi kufurahi! Na mara nyingi anapotoka katika shughuli zake za uvuvi, huwa wanashinda wote wakipeana maneno ya kufarijiana kimapenzi!
Siku zikazidi kusogea mbele, na baada ya Salma kuishi na Karim kwa muda wa miezi kumi, akajifungua mtoto wa kiume. Hakika ilikuwa ni furaha kwa upande wao, na mtoto wakamwita kwa jina la Burhan, jina la babu yake. Hata hivyo, mtoto Burhan alikuwa mweupe sana, kiasi ambacho kilimshangaza sana Karim, kwani alikuwa mweupe kuliko mama yake. Macho yalikuwa ya mng’aro, yaliyotaka kufanana na ya zeruzeru, lakini Karim hakujali hayo, wala kupenda kujiingiza kwenye mambo ya wivu usiokuwa na mfano.
Karim alimpenda na kumthamini mke wake, Salma, kwani aliufuata ule usemi usemao, daima ‘kitanda huwa hakizai haramu, na pia Salma alifika pale akiwa haonyeshi kama alikuwa na mimba. Alionekana ni msichana mzuri, mwembamba wa Kiarabu, basi. Na pengine ni yeye aliyekuwa akishirikiana naye kimapenzi tu, na siyo mtu mwingine!

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...