Ads Here

Thursday, September 26, 2019

*NYUMA YAKO -- 04* *Simulizi za series*

Niliwaza, je watu hawa ndiyo watakuwa na mwili wa Raisi na wale maajenti wa secret service? Nikajikakamua nisimame lakini sikuweza abadani! Sikujua walikuwa wametutilia nini. Nilijihisi mzembe kwa kiwango cha lami! Maungio ya mwili yalikuwa hayajiwezi, mdomo umekauka na masikio nayahisi yamoto!
Kuna muda ulimi nao nilikuwa nauhisi mchungu sana. Nikimeza mate ni kana kwamba yananikaba ama kuniunguza koo! Nilijichukia sana. Kama ningeweza kujitoa kwenye mwili huo, ningefanya vivyo niwe huru. Niliuhisi mzigo.
Kidogo nikawakumbuka wenzangu. Nikajikunja mwili na kuangaza ndani ya eneo tulilopo. Sikuwa naona kitu. Kulikuwa ni kiza tu. Hata nilipokaza macho yangu ya kilemavu kutazama, sikuambulia!
Kwa mbali nilisikia sauti ya mtu akikoroma, ila sikuwa namwona. Nikatamani kumwita mtu huyo, koo likagoma kabisa. Sauti haikuwa inatoka. Nilijitahidi hata nipaze sauti ya kuhema kwanguvu kama ishara lakini ikashindikana, ni kama vile koo lilijawa na vidonda, na mapafu nayo yamesinyaa!
Kusema ukweli sijui ni nini ambacho tulitiliwa. Sijui ni sumu ya namna gani yenye kumtenda mtu vibaya kiasi kile mpaka utamani kufa.
Kwa ustadi wangu wote, sikuwahi kukutana na sumu ile. Nilijiuliza wametumia kitu gani hicho, mti gani? Ua gani? Mmea gani huo? Kweli sikuwa na majibu.
Nilijikuta nikirejea sakafuni na kulala maana hakuna cha maana nilichokuwa nafanya. Kama niko sahihi, baada ya dakika kama tano hivi, nikasikia sauti ya mlango ukifunguliwa. Sikujua kilichoendelea, ila kidogo mkono wangu ukadakwa, nikanyanyuliwa vuup! Nikaburuzwa kupelekwa nje ya jengo tulokuwapo huku watu wawili waliokuwa wananibebelea wakiwa wanaongea lugha nisiyoelewa.
Kama baada ya dakika moja, wakanibwagia chini, pale eneo ambao niliwaona watu wakiwa wanacheza ngoma, kisha sauti nzito ikasema maneno ya ajabu kwanguvu, mara ngoma ikakoma.
Kidogo nikawasikia na wenzangu wakiwa wanatupiwa hapo chini. Bado kulikuwa kimya. Na nadhani tulivyomalizika kutupiwa hapo chini ndipo nikasikia kishindo cha mtu.
Kishindo kilikuwa kikubwa kiasi cha kunifanya niwaze atakuwa ni nani huyo? Mtu mwenye mwili mpana na uzito wa mtoto wa tembo?
Nikadakwa kama kikaratasi na kisha kunyanyuliwa niketi kitako. Nikapanuliwa mdomo na kumiminiwa kimiminika kichungu haswa. Nilipomeza, japo kwa tabu mno, nikaanza kupata ahueni. Kimiminika kile kilinikata sumu kabisa na kunifanya nianze kujihisi ahueni ya binadamu. Macho yalipata uwezo, mwili ukawa na nishati.
Nilistaajabu ni dawa gani ile ambayo iliweza kunipa ahueni haraka vile. Japo nimetumia dawa nyingi za hospitali, sikuwahi kuona ahueni ya upesi kiasi kile. Nilitazama, mbele yangu, nikamwona mtu mmoja mpana kana kwamba mbuyu. Nywele zake zilikuwa nyeusi na ndefu.
Mwili wake umejawa na michoro mbalimbali, shingoni amevalia mkufu wa mifupa ya wanyama na amejisitiri sehemu zake za siri kwa majani yaliyofumwa vema.
Hakuwa na sura ya urafiki. Macho yake yalikuwa makubwa na mekundu yakitingwa na ndita pana kama matuta. Alinitisha. Na namna alivyokuwa ananitazama, nilihisi anataka kunimeza.
Mbali na yeye, watu wengine wote ambao walikuwa wamesimama wakitutazama, nao walikuwa wametukodolea macho. Nao nyuso zao zatisha. Sijui walikuwa wamepakaa nini usoni. Mikononi wamebebelea mikuki mirefu yenye kupambwa na manyoya ya tai. Wanawake kwa wanaume, watoto kwa watu wazima.
Sasa yule mwanaume ambaye amenipatia dawa, mwanaume mpana mwenye uso wa kutisha, akaniuliza, "Sheeta ghasi cha?" Akinikazia macho.
Watu wote walikuwa kimya kana kwamba hamna mtu. Nikatambua kuwa mtu huyu atakuwa ni mwenye nafasi ya juu katika jamii hii. Mtu mwenye kuogopwa na kuheshimiwa. Aidha ni kiongozi au tabibu mkuu.
Lakini lugha aliyoizungumza kwangu ilikuwa mpya. Sikumwelewa. Nilitikisa kichwa na kumwambia kwa lugha yangu kuwa sijamwelewa. Sijawahi kusikia lugha yake hata mafunzoni japo tumesoma lugha kadhaa huko.
Basi mtu huyo akawatazama wenzake na pasipo kusema kitu, mmoja wao akasonga mbele. Huyu alikuwa ni kijana fulani mrefu mwembamba. Nywele zake zilikuwa fupi nyeusi, macho yake makubwa na makali.
Akanitazama, kisha akanisogelea karibu na kuniuliza, "mmetokea wapi? Na hapa mmekuja kufanya nini?"
Nikatambua kuwa kijana huyo alikuwa anazungumza lugha yetu. Nilistaajabu kidogo. Huenda ni mtu ambaye alishawahi kutoka na kwenda kuyajua ya nje ya jamii yao. Kumbe hata yule bwana alipoangaza kando, alikuwa amempa ishara ya yeye kuongea nasi.
Kidogo nikapata tumaini. Kama watatuelewa basi wangeweza kutusaidia na hata kutuachia huru maana hatukuja kuwadhuru bali kutimiza kazi yetu ya msako.
"Tupo hapa kutafuta miili iliyo--"
"Anguka toka kwenye nyota juu?" Akanikatisha kwa swali. Nikamtikisia kichwa, "ndio. Miili iliyoanguka toka kwenye nyota. Nyota ya juu!"
Akamtazama yule bwana mkubwa na kumwambia kwa ile lugha yake. Yule bwana mkubwa akanitazama alafu akaukita mshale wake chini kwa mkono wake wa kushoto.
Akataka kusema nami jambo, akakumbuka hatuelewani, akamtazama yule bwana mdogo na kumwambia nini aniulize.
"Je, mmeshapata mlichokuwa mnakitafuta?"
"Hapana!" Nikawahi kujibu na kisha kuwauliza, "mmeona chochote kile?" Hakunijibu, badala yake akafikisha taarifa kwa yule bwana mkubwa.
Sikujua walikuwa wanawaza nini vichwani mwao, ila walionekana kujawa na mashaka fulani baada ya kuwajibu maswali yao machache. Walijadili kidogo, kama wakielekezana kitu, na mara wakalipuka kwa hasira.
Nikiwa namwona yule bwana mkubwa akiwa amefura, akamimina maneno yake kwa yule bwana mdogo ambaye punde akanieleza kilichosibu.
"Hata kama tungeona kitu, tusingewaeleza. Hatutaki kuhangaika nanyi wauaji na waharibifu wa amani. Tutawaua hivi punde mkawe chakula cha samaki!"
Nikashangazwa, "ni nini kosa letu?" Yule bwana mdogo akafoka akieleza kuwa sisi ni maadui kwao. Tulishawahi kuvamia kijiji chao na kuwamaliza wenzao, ikiwemo kiongozi wao na hata wazazi wa huyo bwana mdogo aliyekuwa mkalimani!
Habari hizi zikanishtua. Na hata kama wale wenzangu wangelikuwa wazima kama mimi, yaani wamepewa dawa ile ya unafuu, wangelishtuka pia. Sikujua ni nini watu wale walikuwa wanazungumzia.
"Hii ni mara yetu ya kwanza kuj--"
"Mwongo!" Nikakatishwa na yule bwana mdogo. Uso wake ulikuwa umebadilika, anang'ata meno na kunitazama kiuchungu.
"Ninyi ni wauaji! Mlidhani tutawasahau? Mlinifanya kuwa yatima, na sasa mmerudi kutuangamiza sote?"
"Sijui nini wazungumza," nikajitetea. "Sijui lolote kati ya hayo mnayotuhusisha nayo. Hatujawahi kuja hapa isipokuwa mara hii..." nikiwa naongea kujieleza, mara watu hao wakaanza kugongesha vitako vya mikuki yao chini na kuimba kwa pamoja "hal! Hal! Hal! Hal!" Sauti yao ilikuwa kubwa kiasi nikaamua kunyamaza maana sikuwa nasikika.
Lakini zaidi nikaogopa maana sikuona kama ni ishara njema. Japo sikuelewa kilichokuwa kinazungumzwa, ila matendo yalinipasha maana. Anamaanisha nini mtu aimbaye hivyo na huku akikata shingo yake kwa kiganja cha mkono?
Tukanyanyuliwa na kutiwa nyavuni,nyavu ngumu iliyotuteka mtegoni, alafu tukaanza kuburuzwa kupelekwa eneo ambalo hatukuwa tunalijua, huko kwenda kuadhibiwa pia kwa kosa tusilolijua.
Tulizama zaidi misituni, mbali na kijiji. Safari nzima wakiwa wanaendelea kuimba "hal! Hal! Hal!" Wakigongesha mikuki ardhini!
Kwa takribani kama dakika nane tukitembea, ndipo wakasimama na kukoma kuimba. Nilipolikagua eneo hilo, nikaona miti mikubwa ikiwa imetengeneza umbo la pembe tatu. Miti hiyo mipana kana kwamba mibuyu, ilikuwa imechorwachorwa sura za ajabu na imefungwafungwa kamba.
Sikufahamu kwanini miti hiyo ilikuwa mikubwa kuliko mingine iliyokuwa imezunguka hapo. Na pia kwa muda huo sikuwa najua kwanini wametuleta kwenye miti hiyo na si mingine. Ila niliwaza pengine ilikuwa ni miti ya madhabahu. Sehemu ambapo wanafanyia shughuli zao za kidini kama vile matambiko na ibada.
Sasa hapo walituleta kutufanyia nini?
Yule bwana mkubwa, kiongozi, akawatazama vijana wanne wa kiume, wakasonga mbele na kutunyaka alafu wakatutia kambani na kutufungia mitini. Wakatukaza haswa kisha wakaimba hapo kwa muda kidogo yule bwana mkubwa akitunyunyizia maji yake ya dawa. Walipomaliza wakaanza kujiondokea.
"Tafadhali msituache hapa!" Nikawaita na kuwasihi. "Hatuhusiki na mlichokisema, tunaomba mtuache huru!"
Hakuna aliyejali, ila yule bwana mdogo alibaki nyuma ya wenzake waondokao. Naye alikuwa wa mwisho akitutazama. Na kabla hajatokomea, akanisogelea karibu na kuniambia,
"Unaona hizo sura mitini, ni za wale tuliowafungia hapa na kuwaacha. Unajua kwanini miti hii ni minene? ... Ni kwasababu inakula watu!" Alafu akatabasamu.
Nikamuuliza, "lakini mbona wewe ni wa tofauti na wenzako? Umejuaje lugha yetu?"
Akaniuliza, "hayo ndiyo maneno yako ya mwisho ukielekea kufa?" Kisha akatikisa kichwa. "Nilidhani wewe ni mwerevu."

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...