Ads Here

Thursday, September 26, 2019

*NYUMA YAKO --- 03* *Simulizi za series

ILIPOISHIA

Hapakuwa na alama ya kitu chochote hapo. Maji yalikuwa yanasukumwa na upepo kutengeneza mawimbi, na miti inatikisika kutengeneza muziki.

Hapa ndiyo nikajua ya kuwa sisi ni watu wa kwanza kufika hapo. Ina maana tangu Raisi aangukie maeneo hayo, hakuna mtu aliyewahi kukanyaga hapo.

ENDELEA

Kidogo nikapata maswali juu ya namna gani jambo hili lilivyokuwa la siri. Siri mpaka pale aidha mwili wa Raisi utakapopatikana au mpaka pale wahusika watakapojulikana. Lakini itachukua muda gani? Hapa nikakumbuka kauli ya Inspector General, kuwa jambo hili haliwezi kukaa kabatini kwa muda mrefu.

Na kwa kuwaza tu, tayari mashaka yatakuwa yameshaambaa miongoni mwa watu. Raisi wa Marekani kutoonekana kwenye mkutano mkubwa kama huo na ingali huku nchini ameshaaga, ni wazi kabisa, ni kitu cha kuzalisha mashaka na maswali.

“Tazama kule!” alisema kamanda mmoja niliyeambatana naye. Tulisonga huko alipokuwa ameelekezea, tukakuta mojawapo ya mabaki ya ndege, kidogo tena tukaona zaidi na zaidi, hapa tukapata maswali, ni kwamba ndege ililipuka kabla ya kuzamia ndani ya maji ama?

Ila hapana. Mabaki haya hayakuonyesha dalili ya kuungua. Huenda wakati ndege inapoteza mwelekeo na kwenda kombo, baadhi ya viungio vyake vilishindwa kukinzana na upepo mkali basi vikabanduka na kunyofoka.

Japo tuliweza kung’amua jambo hilo na kujiaminisha kuwa kweli ndege ilikatiza eneo tulilopo, tukajikuta tukiwa na matumaini mfu sasa juu ya uhai wa Raisi. Ni wazi ndege itakuwa imezama majini, na kwa mahesabu ya kawaida mpaka muda huo tangu tukio litokee, ni ngumu kwa mtu kuwa hai ndani ya maji.

“Sasa tunafanyaje?” akaniuliza mmoja wa kamanda niliyekuwa naye kikosini.

“Tunazama ndani ya maji,” nikamjibu nikimtazama. “Ni lazima tupate mwili wa Raisi, hai au mfu!” nikaongezea taarifa kisha nikatazama huku na kule ndani ya msitu wa kisiwa.

Kulikuwa ni giza na kimya.

Giza na kimya.


**


Sauti ya ndege wa kwanza iliniamsha toka usingizini. Nilijua ni asubuhi sasa japo hakukuwa kumekuchwa na jua. Niliamka na kuangaza, wenzangu walikuwa wamelala. Nikanyanyuka na kuifuata bahari kwa ukaribu. Hapo nikiwa nimeweka mikono yangu mfukoni, nikangaza mandhari, pia nikajiuliza maswali kadhaa ya kipuuzi.

Muda kidogo wenzangu nao wakaamka, basi bila kupoteza muda tukaanza kufanya mpango wa kuzamia ndani ya maji. Wawili miongoni mwetu walikuwa ni watu wenye ujuzi huo, walivalia mitungi ya gesi na vinyago vya majini kisha wakazama.

Tukawangoja kwa takribani lisaa limoja, wakaibuka wakiwa na watu wawili ambao tuliwatambua kama marubani kutokana na sare zao. Kwa kusaidizana, tukapeleka miili hiyo ufukweni.

“Ndege ipo kwenye kina kirefu sana,” alisema mmoja wao aliyezamia. “Yachukua muda kufika na kurudi toka huko, takribani zoezi la dakika ishirini.”

“Hamjauona mwili wa Raisi?” nikawauliza.

“Hapana, hatujauona. Ila hatujamaliza kukagua ndege nzima.”

Wakazama tena, na ikatuchukua kama lisaa lingine kwa wao kuibuka tena juu. Mara hii walikuwa wamewabebelea watu wengine wawili ambao walikuwa wafanyakazi wa ndani ya ndege. Nikawauliza tena kuhusu Raisi, wakanijibu hamna. Hawajamwona.

Nikamwambia mmoja wao, “Nikabidhi nami vifaa nizamie.”

Tukazama humo na mie nikatafuta sana ndani ya mabaki yale ya ndege. Sikuona mwili wa Raisi, zaidi ya kukutana na miili ya watu wengine, wafanyakazi na maajenti wa secret service ambao wanahusika na ulinzi wa Raisi. Nilikaa humo sana nikikagua kila eneo pasipo mafanikio. Mwishowe mpaka mtungi wa gesi ukaanza kuishiwa. Sikuwa na budi kupanda juu kabla mtungi huo haujawa mzigo.

“Vipi, umeona kitu?” akaniuliza mmoja wa wenzangu.

“Hapana,” nikamjibu nikitikisa kichwa. “Nimeambulia hiki tu.” nikawaonyesha tai mkononi mwangu. Wakaichukua na kuitazama. Wote tukakubaliana kuwa tai ile ilikuwa ni ya Raisi. Nyuma yake ilikuwa na bendera na nembo ya Marekani.

“Sasa itakuaje?” akauliza mmoja wao. “Ina maana atakuwa ameangukia kwengine?”

“Inawezekanaje?” nikawahi kutia shaka. “Inawezekanaje aangukie kwengine alafu tai ikabakia ndani ya ndege.”

“Sasa atakuwa wapi?”

“Sijajua,” nikajibu nikiangaza msitu. “Ni ajabu kwake kutoonekana na huku tai kubakia ndani ya ndege! Hii inamaanisha alikuwapo ndani. sasaa …” kwa muda kidogo nikawaza. “Pengine yatupasa kuanza msako wa kisiwa hiki kizima na maeneo yake ya karibu.”

Basi tusipoteze muda tukaanza kufanya hivyo. Tukazunguka kisiwa kizima kwa masaa kadhaa tusione lolote. Hakukuwa na alama yoyote ya binadamu humo. Zaidi tukiwa tunakaribia kufanya kazi yetu hiyo, nikaona mojawapo ya nyayo za binadamu ufukweni. Nikaita na kuwataarifu wenzangu.

“Unadhani itakuwa ni ya nani?”

“Pengine wavuvi. Au wewe unadhaniaje?”

“Wavuvi?” nikapata swali. “Wavuvi tokea wapi?”

Tulipotazama kwa mbali upande wetu wa kaskazini, tukagundua kuwapo kwa kisiwa kingine. Kisiwa hicho kilikuwa kikubwa kuliko hiki cha sasa, nacho kikiwa kimezibwa na misitu ya kijani.

“Twende huko tukatazame,” mmoja akashauri, lakini mimi nikasita, “Sidhani kama Raisi atakuwapo huko.”

“Sasa unadhani atakuwapo wapi?”

“Sijui, ila nahisi ni maeneo ya hapahapa karibu.” nikashauri, “turudi kule kwenye ndege.”

“Kufanya nini huko na tumeshatoka?”

Hapa nilipata shaka na nikajilaumu kwanini mawazo niliyokuwa nayawaza muda huo sikuwa nayo hapo kabla. Nilihisi kuna haja ya kuhesabu wale watu waliokuwemo ndani ya ndege. Juhudi kubwa ni kung’amua kuna maajenti wangapi waliobakia humo ili tutambue kama Raisi alitokomea mwenyewe au alitokomea na baadhi ya maajenti wa secret service.

Tukipata jibu la swali hili basi kwa namna moja ama nyingine tutajua nini cha kufanya. Kufanya hilo vema, tukawasiliana kwanza na kitengo cha Secret service watujuze idadi kamili ya maajenti walioongozana na Raisi, pia wafanyakazi waliokuwamo ndani ya ndege.

Baada ya kujua hilo, tukarejea kule kwenye ndege na kuzamia tena, mara hii nikizama peke yangu kutokana na uhaba wa mtungi wa gesi. Ulikuwa umebakia mmoja ambao ndiyo upo kamili. Nikiwa nafanya hili kwa ustadi, nikagundua kulikuwa na upungufu wa maajenti wawili wa secret service.

Hapa sasa nikapata mashaka. Nao watakuwa wapi? Wameenda na Raisi ama walipotelea maeneo tofauti? Lakini kwanini wao na si wengine?

Maswali haya yalinifanya kichwa changu kiwake moto na hata hatimaye kuishia kuona kuna haja ya sisi kuondoka huko kisiwani ili twende tukatafute majibu nchini kisha tujue namna ya kuenenda.

Lakini kabla ya kwenda huko, nikaona pia ni stara tukaenda kupekua na kisiwa kile ambacho ni kikubwa kipakanacho na hichi tulichopo kwa upande wa kaskazini. Lengo ni kuhakikisha hakuna makandokando yoyote tuliyoyabakiza kwenye eneo la tukio. Tukiondoka basi tumeondoka ‘for good’.

Tukaogelea kwa dakika kadhaa. Tulipofika huko, tukashikilia silaha zetu vema na kuanza kuzama ndani ya kisiwa. Kadiri tulivyokuwa tunazama humo na giza likawa linakua. Miti ilikuwa mingi sana na tena yenye matawi na majani mapana.

Tukatembea kwa muda wa kama dakika nane, mmoja wetu akaona damu ardhini.

“Unadhani kutakuwa na watu hapa?” akauliza. Kabla hatujajibu tukastaajabu nyavu imetusoma na kutukusanya, alafu ikatupeleka juu kabisa ya mti! Nyavu hiyo ilikuwa ngumu haswa na ilitubana mno kiasi cha kuhema kwa tabu.

Tulizama mtegoni! Na hatukuwa na ujanja wowote ule wa kufanya kwani viungo vyote vilikuwa vimebaniwa mwilini. Kurusha macho huku na huku, kidogo tukasikia sauti ya filimbi, na kitu cha mwisho kabisa kukikumbuka ikawa ni maumivu ya kitu kama mwiba mgongoni mwangu. Nikapoteza fahamu.

Nilikuja kugundua baadae ya kwamba tulichomwa sindano za sumu.


**


Nilikuwa kizani sifahamu kinachoendelea, ila kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikaanza kujihisi mwili wangu. Nilijihisi nipo chini tena sina nguo. Mwili unapigwa na baridi kali.

Kichwa nacho kilikuwa kinanigonga, na kwa mbaali nasikia sauti za ngoma. Nikajaribu kufungua macho nitazame. Sikuwa naona vema, nadhani ni kwasababu ya madhara ya ile sumu tuliyochomwa nayo. Nilikuwa naona maruweruwe, watu kama mawingu!

Watu hawa walikuwa wanacheza kwa kuzunguka. Walikuwa wengi na katikati yao kulikuwa na kitu. Ni nini hiki? … nilijaribu kutazama lakini sikuwa naona vema. Mwili ulikuwa mdhaifu na uliochoka sana.

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...