Ads Here

Monday, September 30, 2019

RIWAYA: NI ZAMU YAKO KUFA

SEHEMU YA TANO – PART 1
“Bosi kwani silaha hizo ni za aina gani mpaka waamue kuja kufanyia hapa nchini na si kwao. Na je watu hao ni waafrika au wazungu? Jacob aliuliza huku amekaza macho yake yakitazamana na yale ya Bi. Anita.
“Watu walioingia hapa nchini si wazungu ni waafrika ambao bila shaka wametumika kama vibaraka wa wazungu. Kwa vile silaha hizo ni za hatari sana, ndio maana waliozitengeneza wameogopa kuzifanyia majaribio huko kwao. Kwani taarifa tulizonazo toka Arusha kwa wataalamu wetu zinasema ni silaha za kibaiolojia ambazo huathiri kabisa mfumo mzima wa mwili wa binadamu.
Hivi sasa Ofisi Fukuzi tumeamuliwa na Rais kufanya msako wa watu hao. Polisi wataendelea na uchunguzi wao, ila kama ujuavyo kuwa hiki ni kitengo cha siri sana, hivyo kazi yetu itakuwa huru na siri kama siku zote. Jacob, nataka uende Arusha ukawatafute watu hawa. Kwa kuzingatia muda uliobaki kabla ya mkutano na kasi ya mauaji inayofanywa na watu hao, inahitajika mtu atakayefanya kazi kwa kasi na usahihi mkubwa. Najua unaweza kuwa bado hujapumzika vizuri tangu kwisha kwa ile kazi ambayo ulipambana na Kiroboto, maana ni miezi miwili tu imepita. Lakini nimeangalia nani wa kumpa kazi hii hapa ofisini, nimeona ni lazima mara hii tena nikupeleke Arusha ukatatue suala hili. Ukweli ni kuwa kazi hii inaweza kuwa ya hatari kuliko zote ulizowahi kukutana nazo, kwani hatujui ukweli kuhusu watu hao. Sina hakika kama kweli lengo lao ni kufanya majaribio ya silaha zao tu na si vinginevyo. Hivyo kukutuma wewe ni kama kukupeleka kwa adui ambaye kwa hakika hajulikani undani wake. Lazima ujue kuwa Ofisi fukuzi inakupenda na inakutegemea sana kwa hivyo ningependa ukafanye kazi hii kwa hadhali kubwa.
Si wengi wanaojua kuwa utaelekea Arusha, ninapenda iwe kimya kimya kwani mpaka sasa hatujui adui yetu ni nani. Hivyo kazi yako ni kuhakikisha unaweza kulifikia kundi hili na kulitowesha kabla halijadhuru wananchi wengi zaidi na kuharibu mkutano muhimu kama huu tunaoutarajia ufanyike huko Arusha.
Sitapenda kukupangia namna ya kuondoka wala kuishi kule Arusha, ila naomba iwe siri kubwa. Hii ni kwa usalama wako na wa Ofisi Fukuzi kwa ujumla.
Utapitia gharani kuchukua vifaa unavyodhani utavihitaji katika safari hii. Lakini napenda kukueleza kuwa kuna mtu nimemwandaa kule Arusha ambaye atajitambulisha na utamtambua tu. Yeye ataweza kuwa msaada kwako pindi mambo yakiwa magumu.
Sina mengi ya kukueleza, ila uwe makini, nakutakia kila la heri. Naamini nitapata taarifa kuwa wale watu tayari wako mikononi mwako. Jacob nakuamini na Ofisi Fukuzi inakutegemea” Alimaliza Bi. Anita huku akimpa mkono Jacob
“Asante bosi ila naomba uzidi kuniombea kwani nahisi kila dalili ya hatari ikiwa mbele yangu” Jacob alisema huku akiwa tayari kwa kuondoka.
“Bila shaka Jacob Mungu yuko upande wetu, upande wa haki na watetea wanyonge kama sisi” Hayo yalikuwa ni maneno ya mwisho ya mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi Bi. Anita kwa kijana wake mpelelezi Jacob Matata.
* * *
Alipotoka ofisini kwa Bi. Anita, Jacob alikwenda kilipo chumba cha ofisi yake ndani ya ofisi hizo. Humo alipanga vizuri makablasha yake yaliyokuwa katika mpangilio usiovutia, kisha alikiendea kikasha chake cha siri na kukichukua. Humo alichukua zana kadhaa za kazi na kukirudisha mahali pake.
Baadaye alielekea kwenye kiti na kukaa huku mikono yake ikiwa imepakata kichwa chake. Macho yake yakielekea darini, alikaa hivyo kwa takribani dakika kumi na ushee hivi. Alipokuwa amemaliza kufikiri aliyokuwa anafikiria alisimama na kuweka mikono mfukoni, kabla hata hajapiga hatua moja mara simu yake ya kiganjani iliita. Aliiangalia kama paka aliyeona nyoka akipita. Mtazamo huo ulikuwa wa kiudadisi.
“Nani na nikusaidie nini? Jacob Aliuliza katika sauti yake ya simba.
“Mzee Edson Kinyaro”
Mara moja Jacob alimkumbuka. Huyu mzee ndiye aliyemuokota mtaani na kumtaka akasomee mambo haya ya upelelezi.
“…ni hivi bwana Jacob, kuna mauaji ya kushangaza yanatokea hapa Arusha. Jana usiku aliuawa moja wa majaji wa mahakama ya kimataifa ya Arusha. Jana asubuhi wameuwa watu kadhaa pale Hospitali ya mkoa ya Arusha. Tangu hapo wameshauwawa askari wapatao kumi na mmoja akiwemo, Inspeka wa Polisi Sogoyo.
Kinachoumiza kichwa zaidi ni kuwa zimebaki siku chache ili mkutano huu muhimu wa viongozi wa ukanda huu wa Afrika ufanyike hapa Arusha. Lakini kwa tetesi nilizo nazo ni kwamba mkutano huo upo matatani kufanyika kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kuna barua za vitisho ambazo zimesambazwa na watu wasiojulikana zinatoa vitisho juu ya mkutano huo. Katika taarifa yao hiyo ya vitisho, watu au kundi hilo lisilojulikana limesema kuwa litafanya kitu ambacho kitaacha wazi mdomo wa kila atakayesikia lile watakalolifanya kwa viongozi hao waliopanga kukutana Arusha. Kufuatia barua hizo za vitisho, viongozi wa vikundi na serikali wameanza kutangaza kutohudhulia mkutano huo kwa sababu za kiusalama.
Hebu fikiria kijana wangu jinsi haya mambo yanavyofanyika, inauma sana pale wengine wanapojaribu kujenga na wakati huohuo wengine wanakazana kubomoa na kuharibu. Haijulikani watu hao ni watu gani, wana nia gani na wako chini ya nani. Asante bwana Jacob kwa kunisikiliza, nina imani hutanyamaza na hata kama ukinyamaza, usijali sana nitakuwa nakutaarifu kila mauaji na ubaya utakaokuwa unafanyika”. Alipotaka kukataa simu ndipo Jacob kwa hasira akamwuliza
“Tafadhali, hivi hukuona mtu mwingine wa kumwambia taarifa hizi?
“Wengi nimewaona na nawafahamu, lakini nimeichunguza mikono yao na kutambua kuwa hawangepokea taarifa hizi katika mtazamo na hali ninayotaka waipokee” Alijibu mzee huyo kama mtu aliyekuwa amelitegemea swali kama hilo.
“Bado sijaelewa ni kwa nini umeamua kuniambia mimi wakati kama ni vijana wa nchi wapo wengi sana na ungeweza kuwaambia”
“Bwana Jacob sikusita kukueleza hasa pale nilipokumbuka kuwa wakati serikali inataka kukupeleka kusomea namna ya kutatua masuala kama haya, mimi ndiye niliyetia sahini kuidhinisha fungu la kulipia gharama za mafunzo hayo”
“Sasa mzee Edson, unataka kuniambia kuwa kati ya wote tulioenda kusomae mambo haya umeniona mimi tu?
“Bwana Jacob kumbuka kuwa mlikuwa wengi lakini hamkuhitimu sawa. Kama mlihitimu basi hamkurudi na misimamo sawa. Wengi waliporudi toka kwenye mafunzo, tayari walishakuwa ni vibaraka wa watu fulani wa nchi hizo. Hata kama wapo waliorudi na msimamo kama wako lakini kiutendaji hamko sawa kwani wengine wameshavutwa na nguvu ya pesa. Kumbuka Jacob, haitakuwa na maana pale tutakapokuwa tunatamba kuwa ndani ya nchi yetu tuna mmoja wa wapelelezi wazuri duniani wakati hatupati huduma yake. Najua unajua kuwa kuna kosa la kiufundi lilifanyika miaka ile baada ya Pacha wako wanne kutoweka. Hatukuchukua hatua ya kusafisha. Hao ndiyo wanaosumbua kwa sasa. Nashukuru kuwa ulifanikiwa kumuondoa Kiroboto, ila safari hii kwa mujibu wa taarifa nilizo nazo, Max ndiyo yuko kazini…ameshaacha alama yake ya Sungura aliyefumba macho kila sehemu yalipofanyika mauji….”
“Unamaanisha Max, yule Max “the Fuse”?!!!? Jacob alihamaki.
“Yes, the Fuse himself, yuko ndani ya Arusha, anawasha na kuzima umeme anavyotaka. Jacob mwanangu, siku zote naamini kosa la kiufundi husahihishwa na fundi. Miye kama fundi mstaafu nimeshaliona kosa la kiufundi, ninahitaji fundi alisahihishe, hivyo basi inabidi ufanye kitu, maana kama ujuavyo, Max - the fuse ana uwezo ambao Polisi wa kawaida kamwe hawawezi kumkabili.
Hata hivyo naomba unisamehe kwani sikupiga simu ili kukushurutisha kuacha mipango yako na kuja kutatua jambo hili. Najua umechoka na unahitaji mapumziko kutokana na kazi yako ngumu, hasa ile ya HEKA HEKA. Kwa heri subiri taarifa nilizokuahidi” Mzee Edson Kinyaro alipomaliza tu alikata simu. Bila shaka hakupenda maswali zaidi toka kwa Jacob.
* * *
Wakati Jacob Matata akiwa bado anatafakari taarifa aliyopewa na Edson Kinyaro, huku mkono wa kushoto ukiwa bado umeshikilia simu yake ya kiganjani, huyu yeye alikuwa akipewa mkono wa pongezi na bosi wake. Huyu si mwingine ila ni Max, Max “the Fuse”. Yeye ndiye aliyeteuliwa na vigogo wa mpango wa kuhakikisha mali iliyopo ukanda wa maziwa makuu inaingia mikononi mwa watu wachache. Mpango huu ulikuwa umesukwa na wazungu wachache waliopo katika nchi za magharibi.
Kwa mtazamo wa wazungu hawa walibaini endapo watafika wao wenyewe kuendesha kampeni hii ingewawia vigumu. Hivyo wakaamua kutafuta waafrika wachache wenye sifa wanazozihitaji na kuwakabidhi kazi hii. Kazi ya kuwasafishia njia na kuwawezesha wao kuchukua utajiri uliopo ndani ya eneo la maziwa makuu bila bughuza.
Kazi ya kwanza aliyokuwa amepewa Max ni kuhakikisha anawamaliza wapelelezi wote mashuhuri katika ukanda huu wa maziwa makuu. Kazi hii peke yake ingemwingizia pesa nyingi toka kwa tajiri wake. Pili ingekuwa kuwafyeka viongozi wote ambao wangeonekana kuwa kikwazo katika kufanikiwa kwa mipango ya wazungu hao.
Ni katika kutekeleza kazi ya kwanza, ya kuwamaliza wapelelezi wote mashuhuri katika ukanda huu, ndipo mpango wa propaganda za silaha hatari ulipobuniwa. Hii ilikuwa na lengo la kuhakikisha kuwa wapelelezi wote mashuhuri katika Afrika mashariki watumwe kwenda Arusha ili kwenda kutafuta ukweli juu ya tetesi hizo.
Max kwa ustadi mkubwa alifanikiwa kuingiza vijana wake hatari ndani ya Nchi, huku kwa makusudi makubwa akivujisha taarifa juu ya kuingia kwao hapa nchini.
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...