Ads Here

Thursday, September 26, 2019

Mtego wa Boss Lady.SEHEMU YA KWANZA.

VYUMBA KADHAA VYA KUPANGA MAENEO YA KIJENGE JUU.
CHUMBANI KWA DINO-NJE.
Mlango unafunguka, Dino, kijana Mtanashati wa miaka 22, anatokeza kichwa akiangalia huku na kule kwa sekunde kadhaa, kisha kwa haraka na kwa kunyata anatoka na pole pole na umakini anaufunga mlango huku akihakikisha hakuna sauti inasikika kwa kile anachofanya, pole pole kwa kunyata anaondoka hatua mbili, “unajiona mjanja sio”, sauti nzito ya kike inamshtua Dino na kumfanya ageuke nyuma haraka, anamkuta Mama Tufe, Mama wa makamo wa miaka 68, akiwa amesimama kwenye kona mikono kiunoni uso amekunja mithili ya Mtu anayevumilia maumivu makali ya mwili, mkononi ameshika kofuli kubwa, Dino anashusha pumzi, “Mama pesa yako nitakupa leo jioni” anasema Dino, “nimeshachoka na hizo jioni zako Dino", “jioni ukirudi utanikuta hapa..alafu uanze hizo hadithi zako uone” anasema Mama Tufe na kisha anaondoka akimuacha Dino amesimama pale kwa sekunde kadhaa kabla naye hajageuka na kuondoka.

MTAA WA KALOLENI-BAADAE.
Dino, na Tula, binti mrembo wa miaka 21, wanatembea sambamba, Dino akiwa amebeba Sahani kadhaa, thermos, na vikombe kadhaa, Tula amebeba begi dogo la vitabu, “siku zinakimbia sana” anasema Tula, “mimi nasubiri tu umalize hiyo mitihani tuanze kuishi wote” anasema Dino na kumfanya Tula kushtuka na kugeuka kumuangalia Dino, “wewe ni hicho tu unawaza muda wote Dino” anasema Tula, “badala tuongelee ada ya mtihani ambayo kesho ndio mwisho wa kulipa” anasema Tula, Dino anasita na kuweka vile vyombo chini, anatoa wallet na kutoa noti kadhaa, “usidhani nimesahau Tula” anasema Dino huku akihesabu noti zile, “hizi ni laki na ishirini” anasema Dino huku akimpatia Tula zile pesa, “hiyo inayobaki?” anasema Tula huku anapokea zile pesa, “wewe usiwe na shaka Tula..hilo niachie mimi wewe jiandae na mtihani” anasema Dino huku usoni akionyesha anamaanisha anachokisema, “mpaka jioni nitakuwa na hiyo laki” anaongeza Dino, Tula anabaki kimya kwa sekunde chache kisha anashusha pumzi, “baby nikishindwa kufanya mtihani miaka miwili ya kozi itakuwa imeipotea bure”, anasema Tula huku anaweka zile pesa kwenye mkoba, mara simu ya Dino inaita, anaibofya na kuiweka sikioni, “ndio nipo njiani” anasema Dino na kisha kuitoa simu sikioni, anamuangalia Tula na kumkuta akimkata jicho kali, “nini?” anauliza Dino, “nimesikia sauti ya kike”, “ni Mteja wangu anaitwa Adela..ameniagiza sahani” anasema Dino, “mmh” Tula anaguna, “huamini?” anauliza Dino, “mimi sijasema kitu” anasema Tula, “baby siku nitakusaliti nitajiadhibu kwa kula nusu kilo ya chumvi mbele yako”, anasema Dino na kumfanya Tula kutoa tabasamu kwa mbali na kisha kushusha pumzi, “ok..ngoja mimi niwahi darasani” anasema Tula, “nibusu basi ndio uondoke” anasema Dino na kumfanya Tula kuona aibu akiangalia huku na kule wapita njia kadhaa wanaokatiza maeneo yale, kisha kwa haraka anamsogelea Dino na kumbusu shavuni, Dino anatabasamu huku akimsindikiza Tula kwa macho anavyoondoka.

Dino anainua vyombo vyake pale chini na kuvipanga vyema mkononi na kuanza kutembea,"wee", mara Dino anashtushwa na sauti kali nyuma yake, anageuka na kukutana na Mgambo wa jiji, bwana wa miraba minne, “ulifikiri utatukimbia mpaka wapi kuku wewe?” anasema Mgambo huku akimfikia Dino na kumkwida, “weka vyombo chini na upotee” anasema Mgambo, “hilo halitotokea Mzee” anasema Dino, “unasemaje wewe Mjinga?” Mgambo anasema kwa sauti ya ukali na kitisho, “si umenisikia Mzee” anasema Dino, Mgambo anakwapua zile thermos na vikombe kutoka kwa Dino, Dino anabaki na sahani, “weka hizo sahani chini” anasema Mgambo huku akiwa bado amemkwida Dino shati, Dino anazitupa zile sahani chini na kufanya zipasuke, Mgambo anaziangalia zile sahani pale chini kwa mshangao, “unajua wewe ni pumbavu sana” anang’aka Mgambo,“bora tukose wote” anasema Dino huku akipambana kujinasua kutoka mikono ya Mgambo, hatimaye anafanikiwa kuchoropoka na kukimbia, “we kuja hapa” anasema Mgambo huku naye anakurupuka na kuanza kumkimbiza.

MTAA WA BONDENI-BAADAE.
Dino anatokea kwenye kona akikimbia, anapunguza mwendo huku akiangalia nyuma yake, hamuoni Mgambo, Dino anasimama na kwenda mpaka lilipo jiwe kando ya barabara na kuketi, huku bado akihema kwa kasi, anaketi kwa muda zinapita dakika kama nne hivi, simu inaita, anaitoa mfukoni na kuiweka sikioni, “dada Adela kuna tatizo limetokea nitachelewa kidogo” anasema Dino kwenye simu, “haya mimi bado nakusubiri” inasema sauti ya Adela kisha simu inakatika, Dino anabaki ametulia akionekana kuzongwa na mawazo mazito, zinapita sekunde kadhaa,unasikika mlio wa ujumbe kuingia kwenye simu yake, Dino anaiangalia simu na kuona jina la Tula, anabofya na kusoma ule ujumbe, ‘usisahau ile ahadi Mpenzi’ baada ya kusoma Dino anashusha pumzi nzito na kurudi kwenye utulivu, “nisipolipa kesho miaka miwili ya kozi itakuwa imepotea bure”, Dino anasikia yale maneno aliyosema Tula asubuhi, zinapita dakika mbili hivi, Dino anainuka na kuondoka.

MTAA WA MJINI KATI
Dino anafika na kusimama mbele ya duka moja kubwa la bidhaa mchanganyiko akiangalia meza ya fundi simu iliyo pale pembeni mbele ya duka lile, kukiwa na kibao kinachosomeka, “tunanunua simu mbovu na nzima”, Dino anabaki akiangalia kibao kile kwa sekunde kadhaa kama anayetafakari jambo kwa makini, kisha anaiangalia kwa muda simu yake aliyoibeba mkononi kwake kabla ya kujongea kwenye meza ile, "nauza simu", Dino anasema na kumfanya Jamaa yule aliyeketi pale kuinua kichwa kumuangalia kwa sekunde kadhaa, "hebu niione" anasema jamaa, Dino anampatia Jamaa simu yake ile aina ya Tecno.

CHUMBANI KWA DINO.
Dino anaingia chumbani akionekana amechoka hoi, anaketi pale kitandani, anatoa pesa mfukoni na kuzihesabu noti kumi za elfu kumi kisha anaziweka kwenye stuli iliyo pembeni mwa kitanda chake, “nakusubiri wewe Tula Mpenzi” Dino anaongea mwenyewe kisha anajilaza pale kitandani na kubaki anaiangalia daari ya chumbani kwake, mara anashtushwa na mlango unaogongwa kwa nguvu, “nani?” Dino kwa mshtuko anauliza huku akiinuka pale kitandani, “Mimi” inasikika sauti ya Mama Tufe na kumfanya Dino kuonekana kama Mtu aliyepagawa, “unafungua au nikufungie huko ndani na hili kofuli?” anasema Mama Tufe baada ya kupita ukimya kwa sekunde kadhaa, “nafungua” anajibu Dino huku akichukua zile pesa juu ya stuli na kwenda kuufungua mlango, “elfu hamsini iliyobaki nitakupa kesho jioni” anasema Dino huku akimpatia Mama Tufe zile pesa, “naomba tusitaniane wewe Mtoto” anasema Mama Tufe baada ya kuzihesabu zile pesa, “sikutanii Mama yangu” anasema Dino, “na koma kuniita Mama yako..mimi sio Mama yako” anasema Mama Tufe kwa sauti kali, “kesho ukirudi utakuta kofuli..ukilipa ndio nafungua”, anasema Mama Tufe huku anaondoka, Dino anaufunga mlango na kurudi kuketi pale kitandani akiwa anaonekana kama Mtu aliyechoshwa na safari ya siku nzima.

Zinapita dakika kadhaa kisha Dino anainuka na kutoka.

DUKANI KWA ADELA-NJE.
Adela, dada mrembo wa makamo wa miaka 42, yupo nje ya duka moja zuri la nguo za kike na za Watoto, akimalizia kufunga kofuli kubwa kwenye moja ya mlango wa duka, kisha anageuka na kumuona Dino akikaribia pale alipo, “mbona upo mikono mitupu na simu yako haipatikani?” anauliza Adela, “kuna mambo yamenikuta” anasema Dino, “mambo gani?” anauliza Adela, “mimi ndio nimefunga naondoka..kwa hiyo kama una la kuniambia labda uniambie kwenye gari tukienda” anasema Adela huku akielekea lilipo gari zuri aina ya Toyota Harrier lililopaki pale pembeni, Dino naye anaelekea kwenye gari lile na kuingia, gari linaondoka.

NYUMBANI KWA DINO-NJE.
Anafika Tula akiwa na mkoba wake begani, anafika mlangoni na kugonga mara kadhaa, anatoa simu yake na kuibofya, inasikika sauti inayosema, “Mteja unayempigia hapatikani kwa sasa”, Sura ya Tula inabadilika na kuonyesha huzuni na kukata tamaa, anageuka na kuondoka.

HOTELINI-NDANI.
Adela na Dino wameketi mezani wote wakiwa na vyakula na vinywaji, “hayo matatizo yote yanayokukuta unajitakia Dino” anasema Adela na kumfanya Dino kuacha kula na kumkodolea Adela macho, “kusema ukweli mimi sina shida na vile visahani vyako vya kichina wala mathermos” anaongeza Adela na kumfanya Dino kuongeza butwaa, wanabaki kimya kwa muda, “unaona haya maisha?” anauliza Adela, “hivi ndio nataka uishi” anaongeza Adela, “nenda kakae kafikirie..ukiridhika na nilichokuambia unitafute”, anaendelea kusema Adela huku akipiga funda glasi yake ya mvinyo mwekundu, kinapita kimya kifupi, “mtaji unaotaka utapata na hata mara kumi yake..nitakufungulia duka uuze sahani zako na vikombe na Mgambo hawatokusumbua tena” anaendelea Adela, Dino anabaki kimya kwa muda, kisha anainuka, “subiri” anasema Adela huku anachukua mkoba wake ulio juu ya kiti pembeni, anatoa noti tano za elfu kumi, “nauli” anasema Adela huku akimpatia Dino zile pesa, Dino anasita kwa muda, kisha anapokea na kuondoka.

No comments:

Post a Comment

Chombezo : Penzi La Shemeji Sehemu Ya Pili (2)

Nilishtuka na kutaka kukimbia ila shemeji akanishika mkono "Unakimbia nini?" aliuliza " Hapana sikimbii" nikamjibu ...